•Akizungumza kwenye mahojiano na Tuko TV, Raburu alitoa hakikisho kuwa atapiga hatua hiyo kubwa kabla ya mwezi Desemba.
•Kabla ya kujitosa kwenye mahusiano na Namu, Willis Raburu alikuwa kwenye ndoa na Marya Prudence.
Mtangazaji na mtumbuizaji mashuhuri Willis Raburu na mchumba wake Ivy Namu watafunga pingu za maisha mwaka huu.
Akizungumza kwenye mahojiano na Tuko TV, Raburu alitoa hakikisho kuwa atapiga hatua hiyo kubwa kabla ya mwezi Desemba.
"Huu mwaka bila shaka. Itafanyika kati ya Januari na Desemba, kutakuwa na kitu," alisema.
Mtangazaji huyo mwenye mbwembwe nyingi alimvisha Bi Namu pete ya uchumba mwezi Julai mwaka jana katika karamu iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mwanawe Mali.
Huku karamu hiyo iiyohudhuriwa na wageni waalikwa ikiendelea, Raburu alisimama mbele ya mpenzi wake akiwa ameshika kitu kilichofanana na ua la waridi jekundu kwenye mkono mmoja na kipaza sauti kwenye mkono mwingine.
"Wewe ni mpenzi wangu, wewe ni kila kitu kwangu na itanipa furaha kubwa.." Raburu alimwambia mpenziwe kabla ya kupiga goti na kufungua 'ua' alilokuwa ameshika.
Ndani ya ua hilo bandia kulikuwa na pete ya uchumba.
"...kama wewe Ivy Namulindwa unaweza kuwa mke wake.. tunahitaji jibu," Aliendelea kusema mtangazaji huyo huku akiwa amepiga goti mbele ya Namu.
Namu ambaye alionekana mwenye bashasha kupitiliza hakusita kukubali ombi hilo la ndoa ambalo huenda lilimpata kwa mshangao.
Wageni waliokuwa wamejumuika pale walisherehekea hatua hiyo na kuwapongeza wawili hao ambao hivi karibuni huenda wakafunga pingu za maisha.
Kabla ya kujitosa kwenye mahusiano na Namu, Willis Raburu alikuwa kwenye ndoa na Marya Prudence.
Wawili hao walifunga ndoa mwezi Mei mwaka wa 2017 katika hafla ya kipekee na walitengana mwaka wa 2020.
Wanandoa hao wa zamani walitengana katika hali isiyoeleweka, miezi michache tu baada ya kupoteza mtoto wao.