Willy Paul avunja ukimya baada ya kuachiliwa kutoka kituo cha polisi

Pozee alikamatwa Jumatatu asubuhi nyumbani kwake Syokimau kabla ya kuzuiliwa katika kituo cha polisi kwa muda mrefu wa siku.

Muhtasari

•Willy Paul mnamo Jumatatu jioni aliachiliwa kutoka Kituo cha Polisi cha Karuri Kaunti ya Kiambu alikokuwa amezuiliwa kwa saa kadhaa.

•Wakati akizungumza baada ya kuachiliwa, msanii huyo aliwafahamisha mashabiki wake kuwa yuko sawa na kuwashukuru kwa sapoti yao.

Willy Paul
Image: HISANI

Mwanamuziki mashuhuri wa Kenya Wilson Radido almaarufu Willy Paul mnamo siku ya Jumatatu jioni aliachiliwa kutoka Kituo cha Polisi cha Karuri Kaunti ya Kiambu alikokuwa amezuiliwa kwa saa kadhaa.

Mwimbaji huyo wa nyimbo za mapenzi aliyezingirwa na utata mwingi alikamatwa Jumatatu asubuhi nyumbani kwake Syokimau kabla ya kuzuiliwa katika kituo cha polisi kwa muda mrefu wa siku. Hata hivyo aliachiliwa jioni na kuruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kulipa dhamana.

Wakati akizungumza baada ya kuachiliwa, msanii huyo aliwafahamisha mashabiki wake kuwa yuko sawa na kuwashukuru kwa sapoti yao.

"Nataka tu kusema kwamba ninashukuru kwa sapoti yote na nimenyenyekea. Niko nyumbani salama, Mungu awabariki," Willy Paul alisema katika video ambayo alichapisha ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Msanii huyo wa zamani wa nyimbo za injili hata hivyo hakuzungumza kuhusu kukamatwa kwake wala kufichua kwa nini alizuiliwa katika kituo cha polisi kwa saa kadhaa.

Mwanamke ambaye alidai alidai kuwa wakili anayemwakilisha mke wa Bahati Diana Marua, Bi Caroline Jiseve hata hivyo alidai kwamba Pozee alikamatwa kuhusu  kesi ya unyanyasaji wa mitandaoni aliyoshtakiwa kuhusu takriban miaka mitatu iliyopita,

Wakati akizungumza na wanahabari Jumatatu, Bi Caroline alifichua kuwa ni kesi iliyowasilishwa na mteja wake mwaka wa 2021 ambayo ilimfanya msanii huyo wa zamani wa nyimbo za injili kukamatwa na kuwekwa rumande.

“Mimi ni wakili wa Diana Bahati. Tumekuja hapa kwa sababu ya ripoti ambayo Diana alipeana 2021 kuhusu cyber bullying. Alikuwa ameshtaki Willy Paul ndio maana ameshikwa leo asubuhi, ndio tumemshika,” Bi Caroline alisema.

Akizungumzia kuchelewa kwa kukamatwa kwa msanii huyo, Bi Caroline alidai Willy Paul alikosa kujisalimisha hata  baada ya kuitwa mara kadhaa kufuatia upelelezi kukamilika na maagizo ya kukamatwa kwake kutolewa.

Pia alisema kuwa mwimbaji huyo wa nyimbo za mapenzi mwenye utata atashtakiwa rasmi kortini Jumanne.

“Kesi ya cyberbullying ilikua ile ya 2021 ambayo ilimuathiri Diana na watoto nambayo ilivuma sana, mengine yatajulikana akipelekwa kortini kesho,” alisema.

Vyanzo vya habari vya kuaminika vinasema kuwa Willy Paul aliruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kulipa dhamana ya Ksh100,000.

Mwanamuziki huyo hapo awali alikuwa amedokeza kuhusu polisi waliokuwa wakimtafuta akidaiwa kuwa aligonga mtu. Katika maelezo yake, alikuwa amedai kuwa maisha yake yalikuwa hatarini akitaka polisi wawajibishwe iwapo lolote lingempata.