Zari alilazimika kunyenyekea, kumuomba msamaha mumewe Shakib baada ya Young, Famous & African

Mwanasosholaiti huyo alikuwa na mambo ya kumweleza mumewe Shakib baada ya shoo hiyo kupeperushwa.

Muhtasari

•Zari alikuwa na maelezo ya kumfanyia mumewe Shakib Ijumaa baada ya kupeperushwa kwa sehemu ya pili ya filamu ya Young, Famous na African.

•Haijabainika kama Zari alienda kumwomba radhi Shakib kutokana na kukabiliana kwake na Diamond au nini hasa.

Zari na mumewe Shakib katika eneo la burudani
Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Mwanasosholaiti wa Uganda, Zari Hassan alikuwa na maelezo ya kumfanyia mumewe mdogo, Shakib Cham Lutaaya siku ya Ijumaa baada ya kupeperushwa kwa sehemu ya pili ya filamu ya Young, Famous na African (YFA2).

Sehemu ya pili ya YFA iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na ambayo inawashirikisha mastaa kadhaa wa Afrika iliachiwa Ijumaa asubuhi kwenye Netflix. Mzazi mwenza wa Zari, Diamond Platnumz ni miongoni mwa wahusika wa shoo hiyo kali na wawili hao walikabiliana ana kwa ana katika matukio kadhaa ya filamu hiyo.

Filamu hiyo ya maisha halisi inahusisha maigizo, kufunguka, makabiliano baina ya wahusika kati ya mambo mengine yanayoweza kuvunja ndoa au mahusiano ya wahusika. Haijabainika kama Zari alienda kumwomba radhi Shakib kutokana na kukabiliana kwake na Diamond, kufufuliwa kwa kumbukumbu za mahusiano yao au nini hasa, lakini ni wazi alikuwa na mambo ya kumueleza mumewe huyo wa miaka 31.

"Ninaelekea nyumbani kwa mume wangu kuelezea ni nini hicho kilikuwa  katika #YFA," Zari alitangaza kwenye mtandao wa Instagram Ijumaa jioni na kuambatanisha na video iliyomuonyesha akiendesha gari.

Mama huyo wa watoto watano alisikika akiimba kwa sauti kubwa kwenye video aliyoichapisha.

Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Mapema siku ya Ijumaa, Zari aliwasherehekea wahusika wenzake wote katika YFA2 huku akitangaza kuwa kipindi hicho kingepeperushwa moja kwa moja kwenye Netflix nchini Afrika Kusini mwendo wa saa nne asubuhi.

"Tunapeperusha kuanzia saa nne asubuhi kwa saa za Afrika Kusini #YoungFamousandAfrican," alisema kwenye Instastori.

Aliambatanisha taarifa hiyo na video yake na wahusika wengine wote wakiwa wamekutana katika sehemu moja ambapo Diamond alioneka akiwa amesimama peke yake kwenye kona moja huku akifurahia kinywaji. Video ya mwasosholaiti huyo ilionekana kumwangazia zaidi mzazi huyo mwenzake.

Mkutano wa wahusika wa Young Famous and African huenda ulikuwa mara ya kwanza kabisa wa wapenzi hao wa zamani kukutana baada ya Zari kufunga pingu za maisha na mpenzi wake wa sasa Shakib Cham Lutaaya.

Wahusika wengine ni pamoja na rapa Nadia Nakai, muigizaji Khanyi Mbau, Naked DJ, Swanky Jerry, Kayleigh Schwark, 2Baba na Annie Idibia.