•Zarinah Hassan na Shakib Cham Lutaaya wanatarajiwa kufunga pingu za maisha katika harusi rasmi ya kizungu hivi karibuni.
•Wawili hao walihalalisha muungano wao wa muda mrefu kwa mara ya kwanza katika harusi ya kidini ya Kiislamu (Nikah) mapema mwaka huu.
Wapenzi mashuhuri wa Uganda, Zarinah Hassan na Shakib Cham Lutaaya wanatarajiwa kufunga pingu za maisha katika harusi rasmi ya kizungu hivi karibuni.
Barua ya mwaliko wa harusi ambayo ilifikia Radio Jambo inaonyesha kuwa harusi hiyo itafanyika Jumanne, Oktoba 3 mwendo wa saa sita adhuhuri.
“Zarinah Hassan na Shakib Lutaaya wanakualika kwa moyo mkunjufu kushiriki katika furaha na kusherehekea siku yao ya harusi. Tarehe: 3 Oktoba 2023. Saa: 1200. Uwepo wako kwenye siku hii maalum utafanya sherehe yetu isisahaulike.” ilisomeka barua ya mwaliko ambayo ilitiwa saini na Zari na Shakib.
Hafla hiyo ya harusi itakayofanyika nchini Afrika Kusini itahudhuriwa na wageni wachache tu ambao wamealikwa na maelezo mengi kuihusu yamewekwa faragha. Haijabainika kwanini wapendanao hao wameweka harusi yao kuwa siri kubwa.
Wawili hao walihalalisha muungano wao wa muda mrefu kwa mara ya kwanza katika harusi ya kidini ya Kiislamu (Nikah) mapema mwaka huu.
Wawili hao walifunga ndoa mwezi Aprili baada ya kuwa wamechumbiana kwa takriban mwaka mmoja. Walivishana pete katika hafla ya faraghani ambayo ilihudhuriwa na idadi ndogo ya watu wakiwemo wanafamilia na marafiki.
Picha na video za hafla hiyo iliyofanyika chumbani ambazo zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha wapenzi hao wakiwa wamevalia Kiislamu kabisa huku wakiwa wameketi kwenye mkeka uliotandikwa sakafuni.
Wajati wa hafla hiyo, Shakib alionekana akiinama kwa goti moja na kumvisha Zari pete ya ndoa kwa furaha kabla ya wawili hao kupigana mabusu huku watu wachache waliohudhuria hafla hiyo wakiwasherehekea kwa makofi.
Miezi kadhaa iliyopita, Zari aliweka wazi kuwa alichumbiana na Shakib mara ya kwanza kabla ya kujitosa kwenye ndoa na Diamond Platnumz.
Katika mahojiano, mama huyo wa watoto watano alikiri kuwa amemfahamu mpenziwe mwenye umri wa miaka 31 kwa miaka kadhaa sasa.
Alikiri kwamba yeye na Shakib walichumbiana miaka kadhaa nyuma kabla ya kutengana na kurudiana tena mwaka jana.
"Nilichumbiana na Shakib huko nyuma kisha tukaenda njia tofauti. Sijui tulipatana vipi tena," Zari alisema.
Mzazi mwenza huyo wa Diamond Platnumz alisema haikuwa ngumu kuungana tena na Shakib na kufunga naye ndoa mwezi uliopita kwani waliwahi kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi katika siku za nyuma .
"Mwaka moja baada ya kurudiana alisema nitakufanya mke wangu. Ni hayo tu. Hatukuzungumza kwa muda kisha ghafla mwaka mmoja baada ya kurudiana tukafunga ndoa. Ikiwa sio Mungu, tutaiitaje hiyo?," alihoji.
Zari alirudiana na Shakib mapema mwaka jana baada ya kukatiza mahusiano na mfanyibiashara wa Uganda GK Choppa. Waliweka mahusiano yao siri hadi katikati mwa mwaka jana ambapo walifichua wanachumbiana.