Zuchu ajawa na bashasha baada ya kuzawadiwa na 'mamake' Mama Dangote

"Mamangu Mama Dangote Asante🥰😍," alisema.

Muhtasari

•Zuchu alionyesha viatu vya bluu ambavyo alinunuliwa na mama huyo anayedaiwa kuwa mama mkwe wake.

•Zuchu amechukuliwa kama mwanafamilia wa Mama Dangote huku ikidaiwa yupo kwenye mahusiano na Diamond.

Image: INSTAGRAM// ZUCHU, MAMA DANGOTE

Malkia wa Bongo Zuhura Othman almaarufu Zuchu alishindwa kuficha furaha yake baada ya kuzawadiwa na mamake  Diamond, Mama Dangote.

Kwenye akaunti yake ya snapchat, Zuchu alionyesha viatu vya bluu ambavyo alinunuliwa na mama huyo anayedaiwa kuwa mama mkwe wake.

Katika maelezo ya video, binti huyo wa Khadija Kopa alieleza shukrani zake za dhati kwa Mama Dangote na kudokeza upendo wake kwake.

"Mamangu Mama Dangote Asante🥰😍," aliandika.

Kitendo cha Mama Dangote ni kiashirio tu cha upendo mkubwa na muungano mzuri kati yake na msanii huyo wa mwanawe Diamond.

Image: HISANI

Kwa muda mrefu Zuchu amechukuliwa kama mwanafamilia wa Mama Dangote huku ikidaiwa yupo kwenye mahusiano na Diamond.

Mwezi uliopita, Diamond hata hivyo  kwa mara nyingine aliweka wazi kuwa uhusiano wake na Zuchu ni wa kikazi tu.

Diamond alikana wazi uhusiano wa kimapenzi na mtunzi huyo wa kibao 'Sukari' na kusisitiza kuwa ni msanii wake tu.

Alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya mmoja wa mameneja wake , Hamisi Shaban Taletale almaarufu Babu Tale, kumpa shinikizo kubwa  la kumuoa binti huyo wa gwiji wa muziki wa taarab ,Khadija Kopa.

"Fanya basi uoe unanichelewesha ujue," Tale alimwambia bosi huyo wa WCB chini ya video aliyopakia kwenye Instagram ikimuonyesha Zuchu akimkabidhi mkufu ghali wa dhahabu kama zawadi ya siku ya kuzaliwa.

Diamond ambaye alionekana kutofurahishwa na ujumbe huo wa meneja wake alihoji jinsi angeweza kumuoa msanii wake.

"Sasa nitamuoaje wakati ni msanii wangu Boss?" alihoji. 

Hivi majuzi anayeaminika kuwa baba mzazi wa Diamond, Mzee Abdul Juma Isak, alimshauri bosi huyo wa WCB atafute jiko na atulie sasa.

Mzee Abdul alikosoa baadhi ya masuala katika maisha ya mwanawe ikiwa ni pamoja na hatua yake ya hivi majuzi ya kutobolewa pua.

"Aachane na mambo ya kuiga, aende na maadili ya kitanzania. Kama kuna uwezekano aoe. Pia afuatilie yale ambayo anaweza kuyafanya, asifanye vitu ambavyo vitawashangaza wananchi ama wapenzi wake ," alisema.

Mzee Abdul alibainisha kuwa staa huyo wa Bongo ana uwezo na uhuru wa kufanya jambo lolote atakalo na maisha yake, lakini akamsihi azingatie maadili ya jamii yake ya Kitanzania na ya dini yake ya Kiislamu.