Bosi wa WCB Diamond Platnumz na msanii wake Zuchu wameendelea kuwachanganya wafuasi wao kuhusu hali halisi ya uhusiano wao.
Siku chache tu baada ya kujitambulisha kama mume wa Zuchu, Diamond tena ameonekana na mavazi aliyonunuliwa na malkia huyo kutoka Zanzibar.
Katika ukurasa wake wa Instagram, Diamond alipakia picha kadhaa zinazoonyesha akiwa amevalia T-shati na kofia za manjano, kaptura ya kijani na viatu vyenye rangi nyeupe na mabaka ya kijani.
"Mavazi na Zuchu," Staa huyo wa Bongo aliandika.
Diamond aliendelea kumshukuru binti huyo wa Bi Khadija Kopa kwa mavazi hayo ambayo alionekana kupenda.
"Shukran Zuchu💛," Aliandika.
Ili kuthibitisha kuwa ujumbe huo wa pongezi umemfikia, Zuchu alipakia screenshot ya chapisho hilo la bosi wake kwenye Instastori zake.
Haya yanajiri takriban wiki moja baada ya Diamond kujitambulisha kama mume wa Zuchu chini ya chapisho la WCB kwenye Instagram.
"Huyo ni mume wa Zuuh," Staa huyo aliandika chini ya video ambayo ilimuonyesha akifanya sarakasi mbalimbali jukwaani huku wimbo wake 'Number One' ukicheza.
Siku chache baadae hata hivyo Zuchu alijitokeza kukana kuwa yeye ndiye mhusika aliyeongelewa katika ujumbe huo wa bosi wake.
Akiwa kwenye mahojiano na Wasafi Media, Zuchu alidai kuwa hakuona comment hilo la Diamond na hata kuzua shaka ikiwa kwa kweli ni yeye alitajwa.
"Zuuh wako wengi. Ni kweli naitwa Zuuh lakini si Zuuh mimi, kama ingekuwa mimi angeniambia. Itakuwa Zuuh mwingine," Zuchu alisema.
Mtunzi huyo wa kibao 'Sukari' alisistiza kuwa uhusiano wake na Diamond ni wa kikazi tu.