Esther Musila ahuzunika baada ya kumuacha mumewe Guardian Angel mara ya kwanza

Musila hawajawahi kuwa mbali na mumewe kwa takriban miaka mitatu iliyopita.

Muhtasari

•Musila alifichua kuwa hajawahi kufika ofisini tangu janga la COVID-19 lilipokumba Kenya mwaka wa 2020.

•Musila alifichua kwamba haikuwa rahisi kwake kuwa mbali na nyumbani kwa vile amezoea kuwa na mumewe.

Esther Musila na Guardian Angel
Image: Guardian Angel Instagram

Mke wa mwimbaji wa nyimbo za Injili Guardian Angel, Esther Musila aliripoti kazini leo, Februari 20, kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu.

Akizungumza kwenye video fupi aliyochapisha kwenye mtandao wa Instagram, mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 53 alifichua kuwa hajawahi kufika ofisini tangu janga la COVID-19 lilipokumba Kenya mwaka wa 2020.

Bi Musila alidokeza kwamba amekuwa akifanya kazi kutoka nyumbani katika kipindi cha miaka mitatu ambayo imepita.

"Ni siku nzuri. Leo Februari 20 itakuwa takriban miaka 20 tangu nilipofanya kazi nikiwa ofisini. Leo itakuwa siku ya kwanza," alisema.

Mama huyo wa watoto watatu wakubwa alifichua kwamba haikuwa rahisi kwake kuwa mbali na nyumbani kwa vile amezoea kuwa na mumewe.

Alibainisha kuwa yeye na Guardian Angel hawajawahi kuwa mbali na mwingine kwa takriban miaka mitatu iliyopita.

"Tangu COVID kuanza, tumekuwa pamoja kila siku. Leo ni siku ya kwanza tumetengana. Nitakumiss mpenzi lakini mtu lazima afanye kazi. Acha tuone jinsi itakavyokuwa. Muwe na siku njema," alisema Musila.

Huku akijibu ujumbe wa mkewe, Guardian Angel kwa utani alisema ,"Mumeniharamia bwana."

Wanandoa hao wamekuwa kwenye mahusiano kwa takriban miaka minne na walifunga pingu za maisha mapema mwaka jana.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, Guardian Angel alibainisha kuwa amepata mafanikio mengi katika miaka minne ambayo wamekuwa pamoja.Alitaja uhusiano wake na Bi Musila kuwa muunganisho sahihi.

“Yamebadilisha maisha yangu, ukimsikiliza akiongea (Bi Musila) atasema jinsi mahusiano yetu yamebadilisha maisha yake,” alimwambia Willy Tuva.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 33 alidokeza kuwa athari chanya ya mahusiano yao ndilo jambo muhimu zaidi bila kujali maneno hasi kutoka ya wakosoaji .

Aidha, alifichua kwamba ameweza kukua katika nyanja nyingi za maisha tangu alipojuana na mwenzi huyo wake wa maisha.

“Nimeweza kuwa na ufanisi, nimeweza kukua, sio tu kimwili, lakini nimeweza kukua hata kiuchumi. Hata vitu kama hii ukulima yangu, na sifanyi ukulima kwa shamba ya watu, nafanya kwangu. Hiyo yote imeweza kufanyika kwa sababu ya muungano ambao niko nao na mke wangu," alisema Guardian Angel.

Mapema mwezi huu Musila alimhakikishia mwimbaji huyo wa nyimbo za injili kwamba hana majuto yoyote kwa kuamua kushiriki maisha naye huku akisema kuwa anaweza kufanya hivyo tena na tena.