Fahamu kwa nini Akothee ametakiwa kuandaa karamu yake ya kuhitimu Migori

Akothee amekuwa akifanya Shahada ya Kwanza katika Usimamizi wa Biashara kwa miaka 14 iliyopita.

Muhtasari

•Akothee alifichua atafanya sherehe kubwa mnamo Desemba 10, 2023 baada ya kumaliza kozi yake ya shahada katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya.

•Akothee alisema kuwa wakaazi wa kaunti ya Migori walimuomba afanyie karamu yake huko kwani wangetaka kumsherehekea.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji Esther Akoth almaarufu Akothee ametangaza tarehe rasmi ya sherehe yake ya kuhitimu.

Katika taarifa kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, mama huyo wa watoto watano ambaye amejipa jina la ‘Rais wa Single Mothers’ alifichua kwamba atafanya sherehe kubwa mnamo Desemba 10, 2023 baada ya kumaliza kozi yake ya shahada katika Chuo Kikuu cha Mt Kenya.

Alitangaza kuwa karamu hiyo itaandaliwa katika kaunti yake ya nyumbani, Migori.

"Rais wa Single Mothers, Mtetezi wa maadili ya familia hatimaye amekamilisha shahada yake baada ya miaka 14 💪 Kutokana na Mahitaji ya umma, wakazi waMigori wametaka sherehe ya kuhitumu ifanyike katika Kaunti ya Migori na wala si Nairobi,” Akothee alitangaza.

Aliambatanisha taarifa yake na bango la kutangaza sherehe yake ya kuhitimu ambayo pia itakuwa siku ya Uzinduzi wa shule ya Akothee Academy.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alisema kuwa wakaazi wa kaunti ya Migori walimuomba afanyie karamu yake huko kwani wangetaka kumsherehekea.

"Wanataka kusherehekea Binti yao kwa njia kubwa," alisema.

Aliongeza,”Asante sana MIGORI COUNTY. Mniruhusu niwaonyeshe wasichana wadogo kwamba Elimu ndiyo mali pekee ambayo hakuna mtu anayeweza kukunyang’anya.”

Akothee pia alishukuru Chuo Kikuu cha Mount Kenya ambako amekuwa akifanya Shahada ya Kwanza katika Usimamizi wa Biashara kwa miaka 14 iliyopita.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, mwimbaji huyo alifichua kuwa mama yake ndiye sababu kuu iliyomfanya aamue kurejea chuo kikuu na kufanya digrii yake.

Akizungumza katika TV47 mapema mwezi uliopita, Akothee alisema ingawa alichuma pesa nyingi, maishani mamake hakumwacha apumzike.

"Hivi majuzi nilimaliza elimu yangu ya muda mrefu kutoka Chuo Kikuu cha Mount Kenya na kwa sasa nina shahada. Mama yangu ni mtu wa nidhamu na kila nilipomweleza mafanikio yangu; majumba ninayojenga, hundi zangu benki alibaki nazo. kuniuliza kuhusu shahada yangu," alisema.

Mwanamuziki huyo alisema amekuwa katika chuo kikuu kwa miaka 14 iliyopita na msukumo huo ulitoka kwa mama yake.

"Nadhani nilizaliwa msichana mwenye akilI na ninaamini kuwa sihitaji kusoma vitabU kuandika chochote kwenye karatasi yoyote. Hata hivyo nilihisi kama mama yangu alikuwa shingoni mwangu na ilikuwa bora kupata digrii ili awezE kupumzika," Akothee alisema.