Mwezi Oktoba mwaka jana, malkia wa bongo Zuhura Othman almaarufu Zuchu alimzawadi bosi wake Diamond Platnumz cheni ya thamani.
Cheni hiyo ghali iliyoundwa kutoka kwa dhahabu ilikuwa ni zawadi ya siku ya kuzaliwa ya binti huyo wa Khadija Kopa kwa Diamond.
Hata hivyo, imebainika kuwa kwa sasa mama yake Diamond, Bi Sandra Kassim almaarufu Mama Dangote ndiye anayemiliki cheni hiyo ya gharama yenye kichwa cha bosi huyo wa lebo maarufu ya WCB.
Hivi majuzi, Mama Dangote, kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram alichapisha picha iliyoonyesha baadhi ya mapambo aliyo nayo. Miongoni mwa mapambo hayo, ilikuwa cheni hiyo nzuri ya dhahabu.
"Mama," aliandika chini ya picha hizo.
Katika video nyingine ambayo alichapisha, alionekana akiwa na Esma Platnumz ambaye alimtoa mkufu huo na kuuva shingoni mwake. Katika video hiyo, dada huyo mkubwa wa Diamond alidokeza kuwa staa huyo wa Bongo aligawa zawadi hiyo kwa kuwa kawaida yeye havai mapambo ya dhahabu.
"Kwa nini sasa akupe, sawa, labda kwa sababu havai dhahabu. Sasa inabidi siku ingine inabidi Zuchu amnunulie fedha," alisema Esma.
Mnamo Oktoba mwaka jana, Diamond alionyesha mkufu huo ambao alipewa na Zuchu kama zawadi ya siku ya kuzaliwa.
Kufuatia hayo, Diamond alimshukuru mwimbaji huyo wa kibao 'Sukari' kwa zawadi hiyo na kueleza jinsi anavyomthamini.
"Maneno hayawezi elezea shukran yangu kwa hili Zuuh.. nisije nikatereza kuandika waandishi wakapa kutoa stori bure, ila jua nakushukuru sana, na siku zote utaendelea kuwa pale," aliandika chini ya video ambayo alipakia.
Katika video hiyo fupi, mastaa hao wawili wa Bongo walionekana wakikumbatiana kwa furaha na hata kwa wakati mmoja kubusu midomoni.
Katika kipindi hicho, wawili hao walidaiwa kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa muda mrefu. Binti huyo wa Khadija Kopa na Diamond hata hivyo walitangaza kuvunjika kwa mahusiano yao mapema mwaka huu.
Mwezi Februari, Zuchu aliibua wasiwasi juu ya hali ya mahusiano yake kufuatia chapisho lake kwenye mtandao wa Snapchat.
Mwimbaji huyo wa kibao 'sukari' alidokeza kwamba amevunjwa moyo na mpenzi wake na kutangaza kuwa yuko single.
"Single.." aliandika na kuambatanisha na emoji ya moyo uliovunjika '💔'
Mwimbaji huyo kutoka Zanzibar pia alichukua hatua ya kufuta picha zote za bosi wake Diamond kwenye mtandao wa Instagram.