Fahamu kwa nini familia ya Ally B imeziomba redio, ma-DJ kutocheza nyimbo zake baada ya kufariki

“Msicheze miziki yake tena. Naomba iwe anayetaka, akimkumbuka amtilie dua. Lakini msipige miziki yake!" Kakake Ally B alisema.

Muhtasari

•Kaka wa Ally B alitoa ombi la unyenyekevu kwa vituo vya redio na watumbuizaji kutocheza nyimbo zake baada ya kifo chake.

•Kakake Ally B alisema walitaka roho yake ipumzike kwa amani na kuwasihi wanaotaka kumsherehekea badala yake wamuombee.

Marehemu Ally B
Image: HISANI

Mwili wa mwimbaji mkongwe mzaliwa wa pwani, Ali Khamisi Mwaliguli almaarufu Ally B hatimaye ulizikwa mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Novemba 2.

Marehemu Ally B alifanyiwa ibada ya mazishi ya Kiislamu kabla ya mwili wake kuzikwa katika Maziara ya Cobra, Mishomoroni, Kaunti ya Mombasa. Watu mashuhuri, wanasiasa na mashabiki ni miongoni mwa walioungana na familia, majirani na marafiki wa marehemu mwimbaji huyo kumzika.

Wakati akitoa hotuba yake, kaka wa Ally B alitoa ombi la unyenyekevu kwa vituo vya redio na watumbuizaji kuacha kucheza nyimbo zake baada ya kifo chake.

“Tunaomba news anchors, radio presenters, ma-dj, tafadhali naomba, nyimbo za Ally msicheze. Tafadhali naomba,” kaka wa Ally B alisema.

Alieleza kuwa walitaka roho ya mwimbaji huyo ipumzike kwa amani na kuwaomba wanaotaka kuendelea kumsherehekea badala yake wamuombee.

“Msicheze miziki yake tena. Naomba iwe anayetaka, akimkumbuka amtilie dua. Lakini msipige miziki yake, tafadhali. Twaomba,” alisema.

Kwa niaba ya familia, kaka wa Ally B aliomba vyombo vya habari vipitishe ujumbe huo ili matakwa yao yaheshimiwe.

“Nyimbo zake tosha. Muombeeni lakini msipige miziki yake. Mimi kama ndugu yake nimesema,” alisema.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, muziki, hasa muziki wa kilimwengu, ni haram (ulioharamishwa).

Mwanamuziki anapofariki, kuna imani miongoni mwa Waislamu kwamba muda wowote nyimbo zake zinachezwa au kutumika mahali fulani, hasa kwa madhumuni yanayoenda kinyume na maadili na mafundisho ya Uislamu, ataadhibiwa hata katika maisha ya baada ya kifo.

Kwa mujibu wa jamii ya Kiislamu, muziki hasa wa kilimwengu ni Haramu. Nasema hasa ya kilimwengu kwa sababu baadhi ya wasomi wameeleza kuwa muziki unaokuza amani na usio na nia mbaya au maneno yake unakubalika,” chanzo kimoja cha Kiislamu kilieleza.

Kuna uwezekano kuwa familia ya Ally B waliomba muziki wake usipigwe tena, kwani mwimbaji wa Kiislamu anapoaga, inashauriwa kuwa kazi yote ya kidunia waliyofanya ifutwe kwani inaweza kuwaweka katika hatari ya kuadhibiwa katika maisha yao ya baadaye.

“Kwa Muislamu, kama walikuwa wanafanya muziki, mara baada ya kuaga, inashauriwa kufuta rekodi zao zote na kazi ingine ya kidunia ambayo wanaweza kuwa walitoa kwa sababu kila nyimbo inapochezwa au kutazamwa na mtu ambaye anafanya dhambi kwa kusikiliza muziki wa marehemu, marehemu ataadhibiwa vikali na malaika na hivyo hatakuwa na amani maishani mwake,” kilisema chanzo hicho.

Marehemu Ally B alianza kazi yake ya muziki mwanzoni mwa miaka ya 2000 na alifahamika zaidi kwa nyimbo zake maarufu kama vile ‘Maria’, ‘Bembea’, na ‘Mkufu Wangu’, miongoni mwa nyinginezo.