Gidi ajivunia jinsi mashabiki wanafurahia muziki aliofanya zaidi ya miongo miwili iliyopita

Gidi amezungumzia jinsi mashabiki wanavyomtumia video zao wakifurahia muziki wake kutoka sehemu mbalimbali kote duniani.

Muhtasari

•Gidi alifichua kuwa ni kawaida kwake kupata video kama hizo zikiwa zimetumwa kwenye akaunti yake ya WhatsApp.

•Gidi ambaye alionyesha wazi anajivunia upendo anaoonyeshwa aliahidi kupost video ambazo zitatumwa kwake kama njia ya kuwakubali.

Gidi Ogidi
Image: RADIO JAMBO

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Joseph Ogidi almaarufu Gidi Gidi amezungumza kuhusu jinsi mashabiki wanavyomtumia video zao wakifurahia muziki wake kutoka sehemu mbalimbali kote duniani.

Jumapili asubuhi, mwimbaji wa zamani wa kundi maarufu la Gidi Gidi Maji Maji alishiriki video tatu za mashabiki katika maeneo tofauti wakifurahia wimbo wa ‘I am Unbwogable’ ambao waalifanya takriban miongo miwili iliyopita.

Gidi aliendelea kufichua kuwa ni kawaida kwake kupata video kama hizo zikiwa zimetumwa kwenye akaunti yake ya WhatsApp haswa wikendi.

"Kila Jumapili asubuhi ninapoangalia WhatsApp yangu huwa napata video kutoka kwa watu mbalimbali wanaofurahia muziki wangu mahali fulani ulimwenguni," Gidi alisema.

Akizungumzia video alizoshiriki, alisema, "Kama hili ni tukio fulani mjini Budapest Hungary jana, linalofuata ni Quiver lounge Kilimani, zote zimetumwa kwa wakati mmoja."

Kufuatia hayo, mtangazaji huyo mahiri wa redio ambaye alionyesha wazi kuwa anajivunia upendo anaoonyeshwa na mashabiki kote ulimwenguni aliahidi kuchapisha video ambazo zitatumwa kwake kama njia ya kuwakubali.

“Asanteni kwa upendo, kuanzia sasa nitakuwa nikiweka video hizi kila Jumapili. I AM UNBWOGABLE,” alisema.

Si mara ya kwanza kwa mashabiki kutoka kote ulimwenguni kuonyesha upendo na sapoti kwa mtangazaji huyo wa kipindi cha asubuhi. Amezoea kusifiwa kwa kazi alizofanya miaka ya nyuma na pia anachofanya kwa sasa redioni.

Takriban miezi mitano iliyopita, Gidi alijivunia ubunifu wake baada ya mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu cha Catholic University of East Africa (CUEA) kuwasilisha tasnifu yake kuhusu kitengo cha Patanisho.

Songok Irvine Jepkoskei alifanya utafiti kuhusu nafasi ya redio katika kutatua migogoro ya kifamilia, mfano wa kipindi cha Patanisho kwenye Radio Jambo n mbele ya jopo la wahadhiri.

Alikuwa ameratibiwa kuwasilisha tasnifu hiyo Ijumaa Mei, 5.

Huku akieleza furaha yake kuhusu hatua ya Irvine na kuipongeza, Gidi alimtakia kila la heri mwanafunzi huyo anapowasilisha kazi yake. 

"Leo hii, Irvine Jepksokei kutoka CUEA atakuwa akitetea pendekezo la tasnifu yake kutumia kitengo chetu cha radio Patanisho, tunamtakia kila la heri," Gidi alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Mtangazaji huyo mahiri alibainisha kwamba hii sio mara ya kwanza kwa mwanafunzi kutumia ubunifu wake katika kazi kazi ya shule.

"Mwaka wa 2005, J Nyairo akiwa Afrika Kusini alitetea tasnifu yake ya PhD kutumia wimbo wetu Unbwogable. Tunamshukuru Mola kwa ubunifu," alisema.