Harmonize awakejeli waliozawadiwa maua mnamo Valentine's, Kajala akiwa miongoni mwao

"Na kwa wale waliopata maua , najua sasa yamekauka😅," alisema

Muhtasari

•Konde Boy ameweka wazi kuwa hakumsherehekea mtu yeyote kwani kwa sasa hayupo kwenye mahusiano yoyote.

•Muigizaji Kajala Masanja ni miongoni mwa watu ambao walipokea maua mnamo siku ya Valentino.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize anajivunia kutotumia hata senti moja kwa mwanadada yeyote mnamo siku ya Wapendanao.

Siku ya Jumanne, Februari 14, ulimwengu wote uliadhimisha siku ya Valentine's ambapo wapenzi wengi walichukua fursa kusherehekeana kwa njia tofauti kama vile kuzawadiana, kujivinjari pamoja, kuenda date na nyinginezo.

Konde Boy hata hivyo ameweka wazi kuwa hakumsherehekea mtu yeyote kwani kwa sasa hayupo kwenye mahusiano yoyote.

"Mtumiaji sifuri! 🤑 Hali wakati unapojua kuwa hukununua maua kwa binti ya mtu yeyote !!," aliandika chini ya video yake akiimba na kufurahia wimbo wake mpya 'Single Again' huku akivuta sigara kubwa aipendayo.

Mwimbaji huyo aliendelea kuwashambulia wapendanao huku akiwatania kwamba maua waliyozawadiwa yamekauka tayari.

"Na kwa wale waliopata maua , najua sasa yamekauka😅," alisema.

Aliyekuwa mpenzi wake, Frida Kajala Masanja ni miongoni mwa watu ambao walipokea maua mnamo siku ya Valentino. Jumanne, Muigizaji huyo alionyesha maua ambayo alipokea kutoka kwa moja wa dada zake.

Bintiye Kajala, Paula Paul pia alijigamba na maua na zawadi zinginezo ambazo inaaminika alipokea kutoka kwa mpenzi wake. Paula alipakia yake video akiwa ameshika shada la maua kwenye  mitandao ya kijamii.

Wiki jana, Harmonize aliweka wazi kwamba hayuko kwenye mahusiano yoyote huku akionyesha kujivunia kwake kuwa single.

Katika chapisho kwenye ukurasa wake wa Instagram, Staa huyo wa Bongo pia alidokeza kuwa mama yake alimtahadharisha kuhusu aliyekuwa mpenzi wake. Katika ufichuzi ambao alifanya kama ushauri, bosi huyo wa Konde Music Worldwide  aliwashauri watu kuwapa sikio wazazi wao kila siku.

Harmonize alibainisha kwamba wazazi huwa na jicho maalum la kuwasaidia kuona mambo yaliyofichwa ndani ya mtu.

"Msikilize mama!! Awe ni mama yako mzazi au mama wa mwenzio, baba yako ama wa mwenzio.. wazazi wanakuwanga na jicho la mbali sana. Mzazi ni rahisi kugundua kila kitu. Inawezekana ukawa unajiona unajua kila kitu kumbe kuna jicho la mama. Akiangalia kitu au mtu anapata jibu sahihi kuliko wewe," alisema.

Kajala alitangaza kuhusu kuvunjika kwa mahusiano yake ya miezi kadhaa na Konde Boy mapema mwezi Desemba.

Ingawa hakuweka wazi kilichowatenganisha, alibainisha kuwa hakubeba kinyongo dhidi yake licha ya mahusiano kugonga mwamba.

Mimi kama mwanamke na binadamu nimeumbwa kupenda na kusamehe pia, ila kwenye hili nastahili kuchekwa, nastahili kubezwa na kudharauliwa pia. Sipo hapa kujitetea wala kutia huruma ni kweli nilifanya makosa na nimeyagundua makosa yangu, mimi siyo mkamilifu," Kajala alisema mwezi Desemba.

Mama huyo wa binti mmoja aliweka wazi kwamba alikuwa tayari kupiga hatua nyingine baada ya mahusiano kusambaratika.