Harusi tunayo! Nandy azidiwa na hisia baada ya kufunga pingu za maisha na Bilnass

Ni rasmi kuwa Bilnass na Nandy sasa ni mume na mke.

Muhtasari

•Wasanii hao wawili kutoka Bongo walifunga pingu za maisha ndani ya kanisa mnamo Jumamosi, Julai 16.

•Nandy alionekana kuwezwa na hisia huku akitoka nje ya kanisa akiwa ameshikana mkono na mumewe.

wamefunga pingu za maisha mnamo Julai 16, 2022
Bilnass na Nandy wamefunga pingu za maisha mnamo Julai 16, 2022

Ni rasmi sasa kuwa Bilnass na Nandy ni mume na mke.

Wasanii hao wawili kutoka Bongo walifunga pingu za maisha ndani ya kanisa mnamo Jumamosi, Julai 16.

"Bi William Nicholaus Lyimo👸," Nandy alijitambulisha kwenye mtandao wa Instagram baada ya harusi.

Harusi kati ya wawili hao ambayo ilikuwa imesubiriwa kwa hamu na ghamu ilifanyika katika kanisa moja lililo eneo la Mbezi Beach.

Wanafamilia, marafiki na hata mashabiki walishuhudia wapenzi hao wakivishana pete na kula kiapo cha ndoa.

"Pokea pete hii, iwe ukumbusho na alama ya ahadi ya ndoa hii kati yako nami, nakuwa mwaminifu kwa ndoa hii mpaka kufa," Bilnass alimwambia mkewe.

Nandy pia alikula kiapo kama hicho huku akimvalisha mumewe pete ya ndoa.

Mamia ya washirika waliokuwa wamejumuika pale kanisani walishangilia kwa sauti baada ya wawili hao kuvishana pete.

"William ameoa leo," Mtumishi wa Mungu aliyesimamia wawili hao wakifunga pingu za maisha alisema.

Baada ya kuwaunganisha wawili hao kwa kifungo cha ndoa,  kasisi aliwakabidhi cheti cha ndoa. Aliendelea kuwapa maneno mafupi ya ushauri na kuwaalika kanisani.

Wanandoa hao wapya mjini waliwageukia washirika na kuonyesha cheti chao cha ndoa kabla ya wazazi wao kualikwa jukwaani.

Wakati ibada ya harusi illisha Nandy alionekana kuzidiwa na hisia na hata kuangua kilio cha furaha huku akitoka nje ya kanisa akiwa ameshikana mkono na mumewe.

Tunawatakia wawili hao ndoa yenye fanaka na furaha tele!