Huwa sivai chupi za Kenya, nikifariki nizikwe katika mavazi yangu ya harusi- Akothee

Akothee alisema amekuwa kwenye ndoa 3 pekee, akiwa ameolewa rasmi na mwanamume mmoja tu.

Muhtasari

•Akothee aliwasili nchini Alhamisi akiwa amebeba bidhaa mbalimbali ambazo aliweza kununua barani Ulaya wakati wa ziara yake.

•Alitangaza kuwa harusi yake ya pili itakuwa tukio kubwa huku akibainisha kwamba anapanga kusherehekea kwa mwaka mzima.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki Esther Akoth almaarufu Akothee alitua nchini siku ya Alhamisi asubuhi baada ya ziara yake ya siku kadhaa barani Ulaya.

Akothee ambaye alizuru mataifa ya Ufaransa na Uswizi katika kipindi cha wiki moja iliyopita aliwasili katika uwanja wa ndege wa JKIA akiwa amebeba bidhaa mbalimbali ambazo aliweza kununua barani Ulaya wakati wa ziara yake.

Akizungumza na wanahabari, aliweka wazi kwamba alisafiri kwa ajili ya kununua mavazi yake muhimu yakiwemo gauni la harusi ijayo na chupi huku akibainisha kwamba kwa kawaida huwa ananunua mavazi yake ya ndani nje ya nchi.

"Nilikuwa nimeenda kununua nguo zangu za ndani kwa sababu huwa sivai kutoka hapa Kenya kusema ukweli. Hizo ni vitu muhimu sana kuzingatia. Kubwa kabisa ni gauni langu la harusi kwa sababu nilitafuta nikakosa," alisema.

Mwimbaji huyo alidokeza kwamba harusi yake ambayo imeratibiwa kufanyika mnamo siku yake ya kuzaliwa itakuwa hafla kubwa ya kipekee.

Alibainisha kwamba maandalizi makubwa yanaendelea kufanyika kwa ajili ya siku hiyo kubwa katika maisha yake na kufichua kuwa hafla hiyo imegharimu kiasi kikubwa cha pesa kuanzia kwa mavazi, vyakula na maandalizi mengine.

"Gauni limenigharimu 4,800 Swiss Francs  (Ksh 693, 000). Duka ambalo nilienda ni la hali ya juu, viatu ni 1,200 Swiss Francs (Ksh 173, 000). Ni viatu vya harusi ambavyo unaweza kusimama siku nzima ukiwa nazo," alisema.

Akothee aliweka wazi kwamba alitumia pesa zake mwenyewe kununua mavazi hayo ya harusi yake itakayofanyika hivi karibuni.

Alidokeza kuwa hafla hiyo itakuwa ya kuvutia na yeye haswa ataonekana wa kupendeza sana katika mavazi yake ya harusi. Aidha, alisema angependa kuzikwa akiwa amevalishwa mavazi atakayovaa siku ya harusi yake. 

"Najua watu hawapendi kuzungumzia kifo. Lakini nitakuwa nimepatia familia yangu kazi rahisi sana. Hivyo ambavyo nitakuwa nimevaa mnamo siku yangu ya harusi, ningependa nilale hivyo hivyo. Nikipumzika, nizikwe ndani ya vitu nitakuwa nimevaa siku ya harusi," Mwanamuziki huyo alisema.

Mama huyo wa watoto watano alitangaza kuwa harusi yake ya pili itakuwa tukio kubwa katika maisha yake huku akibainisha kwamba anapanga kusherehekea kwa mwaka mzima.

Pia aliweka wazi kuwa amekuwa kwenye ndoa tatu pekee kufikia sasa, akiwa ameolewa rasmi na mwanamume mmoja tu, Bw Jared Okello, baba wa binti zake watatu wa kwanza.