"Huyu roho imependa!" Jimal asifia mahusiano yake mapya, adokeza mpenziwe kuchora tattoo yake

"Huyo ndiye baby girl. Hao wengine ni stori iliyopita," alisema.

Muhtasari

•Jimal alidokeza kuwa mzazi huyo mwenzake mtarajiwa atachora tattoo ya jina lake kama alivyokuwa amefanya Amber Ray.

•Ingawa bado hawajampokea mtoto wa kwanza, Jimal alidokeza mpango wa kuongeza watoto wengine wawili na mpenziwe.

Image: INSTAGRAM// JIMAL ROHOSAFI NA MICHELLE WANGARI

Mfanyibiashara na Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa Matatu jijini Nairobi, Jimal Marlow Rohosafi, ameshikilia kwamna rafikiye wa muda mrefu, Michelle Wangari ndiye mpenzi mpya wa maisha yake.

Akizungumza na kituo kimoja cha redio cha hapa nchini, baba huyo wa watoto wawili aliweka wazi kuwa tayari amezama kwenye dimbwi kubwa la mahaba na mzazi huyo mwenzake mtarajiwa.

"Huyo ndiye baby girl. Hao wengine ni stori iliyopita," alisema. 

Wakati huo huo, Jimal alithibitisha kwamba kwa kweli anatarajia mtoto wa kwanza na mpenzi huyo wake.

"Tushajua jinsia ya mtoto. Huyu roho yangu imependa. Huyu ni yeye!" alisema kwa sauti iliyojaa kujiamini.

Mfanyibiashara huyo alibainisha kuwa yeye na Bi Wangari wanapendana sana na hata kudokeza kuwa mzazi huyo mwenzake mtarajiwa huenda akachora tattoo ya jina lake kama alivyokuwa amefanya Amber Ray.

"Ni tattoo tu hajaweka, lakini ataweka hivi karibuni" 

Ingawa bado hawajampokea mtoto wa kwanza, Jimal alidokeza mpango wa kuongeza watoto wengine wawili na mpenziwe.

"Huyu roho yangu imependa. Naweza kuongeza mwingine wa pili na wa tatu," alisema.

Baba huyo wa watoto wawili alibainisha kuwa hana mawasiliano mengi na aliyekuwa mke wake, Amira. Hata hivyo alifichua kuwa anaendelea kushirikiana na mzazi huyo mwenzake katika malezi ya watoto wao.

Jimal alisema hajakatiza mawasiliano na Amira tu bali pia na aliyekuwa mkewe wa pili, mwanasoshalaiti Amber Ray.

"Sijawablock (Amira na Amber Ray), lakini hatuongei, Tukiongea huwa tunazungumza mambo ya watoto, basi," alisema.

Wakati huo huo, mfanyibiashara huyo alimshtumu Amira kwa kuendeleza vitendo vya kishirikina huku akidai kwamba mke huyo wake wa zamani alikuwa akimroga wakati walipokuwa kwenye ndoa.

Jimal aliweka wazi mahusiano na Wangari mnamo siku ya Wapendanao huku akifichua kwamba wanatarajia mtoto pamoja.

"Nilisema nitapenda baada ya miaka mitatu na nikama imenda haraka.❤️ #hiimenda," mfanyibiashara huyo aliandika kwenye picha ya yeye na mpenzi huyo wake ambaye alionekana mjamzito.

Kwa upande wake, Michelle alibainisha kuwa kupata mtoto pamoja ni uamuzi bora ambao aliwahi kufanya na mpenziwe.

Pia alidokeza kuwa uhusiano wao umedumu zaidi ya mwaka mmoja huku akisherehekea siku ya kumbukumbu ya mahusiano yao.

"Tunasherehekea zaidi ya Siku yetu ya Wapendanao, uamuzi bora zaidi ambao tumewahi kufanya ni kuwa na wewe ❤️. #happyanniversary mpenzi wangu," Michelle aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Jimal alitemwa na  Amira, mwishoni mwa mwaka 2021 baada ya kuhusika kwenye mzozo wa mapenzi kwa muda mrefu. Baada ya kumtema mfanyibiashara huyo, Amira alielekea mahakamani kudai talaka.