logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Inspekta Mwala avunja kimya kuhusu tetesi kwamba amefariki

Mwala ameichua kwamba tayari amechukua hatua ya kisheria na kumshtaki mhusika kwa DCI.

image
na Samuel Maina

Burudani07 January 2023 - 10:10

Muhtasari


  • •Akaunti ya Tiktok ilichapisha video ya mkusanyo wa picha za mchekeshaji huyo na kudai kuwa alifariki asubuhi hiyo.
  • •Mchekeshaji huyo alifichua kwamba tayari amechukua hatua ya kisheria na kumshtaki mhusika kwa DCI.

Muigizaji na mchekeshaji mkongwe Davis Mwambili almaarufu Inspekta Mwala amejitokeza kukanusha madai ya kwamba amefariki.

Mwala ambaye anajulikana zaidi kutokana na kipindi cha Inspekta Mwala kwenye Citizen TV amelazimika kuweka mambo wazi kuhusu uvumi huo baada ya video inayodai kuwa alikata roho kusambaa  kwenye mitandao ya kijamii.

Siku ya Alhamisi, akaunti ya Tiktok ilichapisha video ya mkusanyo wa picha za mchekeshaji huyo na kudai kuwa alifariki asubuhi hiyo.

“RIP Mwala, amefariki asubuhi ya leo,” maelezo ya video hiyo yalisomeka.

Mwala hata hivyo amejitokeza kulaani  mtumizi wa Tiktok aliyechapisha video hiyo na kusema kwamba alichofanya ni kumuua akiwa hai.

Akizungumza na Citizen Digital, mchekeshaji huyo alifichua kwamba tayari amechukua hatua ya kisheria na kumshtaki mhusika.

"Mwala bado yuko hai, yeyote aliyetengeneza klipu hiyo atahadhari kwa sababu nimeripoti kwa DCI na haitakuwa nzuri tutakapokutana nao," alisema.

Mchekeshaji huyo mkongwe alibainisha kuwa sio mara ya kwanza kwa habari za uongo kuhusu kifo chake kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

" Wakati huu ilikuwa TikTok, mwaka jana ilikuwa Facebook, wakati mwingine Twitter….inahitaji kuacha," Inspekta Mwala alisema.

Mwaka wa 2018, uvumi kwamba Mwala ameaga dunia ulisambaa kwenye mitandao ya kijamii baada ya muigizaji huyo kuhusika katika ajali mbaya ya barabarani kando ya barabara ya Mombasa.

Ajali ya Inspekta Mwala ilitokea alipopoteza udhibiti wa gari lake aina ya Toyota Lexus alipokuwa akiendesha kutoka Nairobi kuelekea Machakos na kusababisha gari hilo kugonga nguzo.

Alipata majeraha na kulazimika kukimbizwa katika hospitali ya karibu katika eneo la  Athi River. Kwa kuwa hali yake ilikuwa mbaya, baadaye alihamishiwa katika hospitali ya Agha Khan jijini Nairobi.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved