Mbunge wa Lang'ata Phelix Odiwour almaarufu Jalang'o amezungumza kuhusu kifo cha marehemu mwanatiktok Brian Chira.
Jalang'o alikuwa kwenye RahaFest mnamo Jumamosi, Machi 30 ambapo aliulizwa maoni yake kuhusu kilio cha Chira cha kuomba msaada kuhusu shida mbalimbali alizokuwa akikabiliana nazo.
Aliiambia Plug TV Ke kuwa;
"Inaniuma sana kuwa baada ya kifo cha Chira, niliona video akisema kuwa Jalango I need your help. I need you to help me. Niliona baada ya kifo chake, ndio watu wengine wali tag mimi. How I wish ningekuwa nimeiona," alisema.
Jalang'o aliendelea kusema, "Ningekaa na kumuuliza unataka nini. Inaniuma sana kwamba niliona hiyo video baadaye sana."
Mwanasiasa huyo alitoa heshima za mwisho kwa marehemu TikToker huyo.
"Mungu ailaze roho yake katika amani ya milele," Jalang'o aliomboleza, akitoa wito kwa wabunifu wa Kenya kuhakikisha jina zao zinaishi zaidi.
"Leo wewe ni msanii wa juu, kesho wewe ni mtu mwingine."
Kuhusiana na malalamiko kwamba waombolezaji walifanya vibaya wakati wa mazishi ya Chira, Jalang'o alisema kuna somo la kujifunza.
"Ujana Moshi. Na inapita sana. Ni vijana tu na lazima tukubali ni vijana. Huwezi kuwaouuza wanatiktok leo."
Alisifu jamii ya TikTok kwa kuchangia pakubwa katika gharama za mazishi ya Chira. "Kuna mazishi ya watu wakubwa leo ambapo wanahangaika kupata hata milioni moja. Lakini wanatiktok walichangisha Sh8 milioni. Si kundi unaloweza kulipuuza."
"Kama kifo cha Brian Chira hakikuwahi kukufundisha chochote basi huwezi kufundishwa. Kifo cha Brian Chira ni somo kubwa sana. Watakupenda wengi sana kama hauko, na wakati unapopiga nduru ukiwa jangwani na kuitisha maji wengi hawatakupa maji. Ukisha kufa watakuletea kisima. Hata bahari," alipima uzito.
Aliongeza kuwa maisha na nyakati za Chira zinapaswa kuwa wakati kwa wote kutafakari urafiki wa kweli.
"Usije ukafikiri siku moja mjai hauwezi kumyonga mamba."