Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa amewataka Wakenya kutomhusisha mchekeshaji Jasper Muthomi almaarufu MC Jessy na jamii ya LGBT.
Siku ya Jumanne, Jessy ambaye aliwania kiti cha ubunge cha Imenti Kusini katika uchaguzi wa Agosti mwaka jana alizua maswali mengi baada ya kuchapisha picha yake akiwa amevalia sketi kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Pichani, mchekeshaji huyo wa Churchill Show pia alikuwa amebeba begi ndogo ya kufungwa kiunoni ambayo kawaida hubebwa na wanawake.
"Wale mnajua sana, Hii bag ni ya nini?" aliuliza kwenye Instagram.
Mamia ya wanamitandao walitoa maoni tofauti, baadhi yao wakikejeli mtindo wake wa kuvaa, wengine wakiusifia huku wengine wakimkosoa mchekeshaji huyo mwenye uzoefu mkubwa kwa "kuvaa nguo za kike.''
Baadhi ya wanamitandao pia walimhusisha na jamii ya wapenzi wa jinsia moja ambayo imekuwa ikiangaziwa sana katika siku za hivi majuzi kufuatia mauaji ya kinyama ya mtetezi wa jamii hiyo, Edwin Chiloba.
Mbunge Barasa hata hivyo amesema mavazi ambayo Jessy alikuwa amevalia ni ya kitamaduni nchini Scotland kwa wanaume.
"Wadau hii haijaenda. Mtindo huu wa mavazi ni mtindo wa mavazi ya kitamaduni nchini Scotland kwa wanaume. Huvaliwa wakati wa siku muhimu sawa na siku ya huduma nchini Kenya," alisema kupitia mtandao wa Facebook.
Barasa alisisitiza zaidi kuwa mchekeshaji huyo ambaye alikuwa na matamanio ya kugombea ubunge kwa tiketi ya UDA si shoga.
"Naweza kuthibitisha kuwa MC Jessy (Jessy Jasper) si mwanachama wa LQBTQ ama inaitwaje ...ile ya kugeuzana," alisema na kuambatanisha ujumbe wake na picha ya mchekeshaji huyo akiwa amevalia sketi.