•Karen Nyamu amebainisha kuwa DP Rigathi Gachagua alikuwa sahihi kumsuta hadharani mpenzi wake Samidoh mapema mwaka huu.
•Hali kama ile iliyotokea Dubai haikuwa mzaha, ilikuwa mbaya na ilikuwa kuteleza kwa sehemu yake (ya Samidoh)," Karen Nyamu alisema.
Seneta wa kuteuliwa Karen Njeri Nyamu amebainisha kuwa naibu rais Rigathi Gachagua alikuwa sahihi kumsuta hadharani mpenzi wake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh mapema mwaka huu.
Mwezi Januari mwaka huu, naibu rais alipokuwa akitoa hotuba yake katika hafla, alimtaka staa huyo wa Mugithi kuchukua udhibiti kamili wa mahusiano yake kufuatia tukio baya lililotokea jijini Dubai mwishoni mwa mwaka jana ambalo lilimhusisha yeye, mke wake wa kwanza Edday Nderitu na Karen Nyamu.
Katika kauli yake, DP Gachagua alisema kuwa mwanamuziki huyo amepata heshima ya wengi kupitia tungo zake za muziki na ni wakati wake sasa kurejesha utulivu katika familia yake na kuhakikisha adabu inatawala.
"Sasa wewe Samidoh ucontrol watu wako. Panga panga hiyo maneno yako na ukishindwa, tutakukataza kwenda kwenye wimbo," Gachagua alimwambia Samidoh kwa utani wakati wa ibada ya mazishi ya dadake waziri Moses Kuria, Pauline Nyokabi.
Katika mahojiano ya hivi majuzi kwenye chaneli ya YouTube ya Convo, seneta Karen Nyamu alimtetea naibu rais akisema kuwa alikuwa sahihi kumtaka mzazi mwenzake kudhibiti nyumba yake.
Mama huyo wa watoto watatu alikubali kwamba tukio la kusikitisha lililotokea jijini Dubai lilikuwa kuteleza kwa upande wa Samidoh.
“Si mzaha. Hali kama ile iliyotokea Dubai haikuwa ya mzaha, ilikuwa mbaya na ilikuwa kuteleza kwa sehemu yake (ya Samidoh)," Karen Nyamu alisema.
Aliongeza, "DP alikuwa akimsuta kwa sababu ilikuwa ni upotovu kwa upande wake kabisa."
Mwezi Desemba mwaka jana, video ilisambaa mtandaoni ikimuonyesha Nyamu na mke wa Samido Edday wakipigana vibaya kwenye tamasha jijini Dubai ambapo Samidoh alikuwa akitumbuiza.
Mzozo kati ya wawili hao ulishuhudia Nyamu akitolewa kwa nguvu kutoka kwa jukwaa na kufukuzwa na mlinzi.
Katika klipu tofauti, Nyamu alirekodiwa akicheza jukwaani huku Samidoh na mwimbaji wa nyimbo za injili Karangu Muraya wakitumbuiza.
Wakati huo ndipo seneta huyo wa kuteuliwa alipofukuzwa baada ya ugomvi mwingine kutokea.
Wakili huyo baadaye alilaumu matendo yake kwa pombe, tabia ambayo aliapa kuacha kuanzia Januari mwaka huu.