Masaibu ya wasanii chipukizi nchini Kenya

Serikali inapaswa kujipiga msasa na kuwapa viijana motisha kwa kuwa vijana ndio nguzo ya jamii

Muhtasari

• Kutokana na ufisadi uliokithiri katika kila pembe ya nchi na wizara husika, inakua ni muhali sana kwa wasanii hawa kupata fursa ya kujiendeleza kiusanii

•Wengi wanamalizia kutafuta njia mbadala za kujimudu kimaisha nao wengine kumalizia katika maovu na anasa

• Iwapo taifa litasimama kidete basi vipawa mbalimbali vitachipuka 


Taasisi ya kukuza talanta
Image: MAKTABA

Ni suala linalozidi kuzusha mijadala mbalimbali iwapo Kenya imeipa kipaumbele sanaa na tamasha tofauti tofauti ili kukuza talanta za wasanii.

Baadhi ya wasaniii chipukizi wamezidi kulemewa na hali ngumu ya maisha inayowakumba kila kukicha kutokana na ukosefu wa miundomisingi  mwafaka ya kukuza talanta zao.

‘’Kuna tofauti sana kati ya msanii mkuu na msanii chipukizi. Msanii mkuu ana uwezo wa kujimudu kimaisha kwa kuwa amejiunda kimuziki ilhali msanii chipukizi apo kwenye pilkapilka za kujiunda ili kujimudu kimaisha,’’ alinena hivyo msanii chipukizi Derrick Obwangi almaarufu AMUH JR.

‘’Kenya ina wasanii ghaya chungu nzima tukianzia viwanjani hadi hewani ila kutokana na ufisadi uliokithiri katika kila pembe ya nchi na wizara husika, inakua ni muhali sana kwa wasanii hawa kupata fursa ya kujiendeleza kiusanii.''

''Hivyo basi wengi wanamalizia kutafuta njia mbadala za kujimudu kimaisha nao wengine kumalizia katika maovu na anasa,’’ alizidi kusisitiza AMUH JR kwa hamaki na simanzi.

‘’Ni bayana kwamba Kenya huwa imetenga mamilioni ya masarafu hasa katika kitengo hiki cha usanii kupitia taasisi ya MUSIC COPYRIGHT SOCIETY OF KENYA (MCSK) ila hela hizi hazipati kuwafikia wasanii chipukizi,’’aliendelea kutamba AMUH JR akiwa amesononeka.

Yakini serikali inapaswa kujipiga msasa na kuwapa viijana motisha kwa kuwa vijana ndio nguzo ya jamii. Vilevile vijana ndio uti wa mgongo wa nchi kutokana na huduma wanazozitoa katika ujenzi wa taifa.

Hivyo basi ni jukumu la viongozi na taasisi husika kujitoma ulingoni na kusimama kidete ili kukimu matakwa ya nguzo hii muhimu ya jamii.

Mbali na hayo ni jukumu la vijana kujitoma katika ujenzi wa taifa kupitia sanaa na talanta kwani mataifa ya ughaibuni yameipa kipaumbele sanaa za vijana na wasanii chipukizi ili kujimudu kimaisha.

Ikumbukwe kuwa heri nusu shari kuliko shari yenyewe,yaani, heri kidogo kuliko kukosa. Iwapo taifa litasimama kidete basi vipawa mbalimbali vitachipuka na ukuaji huu utachangia pakubwa ukuaji wa uchumi katika taifa la Kenya .