Kijana apatikana amefariki nyumbani kwa Mwimbaji wa Mugithi, suruali yake ikiwa chini

Kabla ya kukumbana na kifo chake, Mwathi kwa bashasha tele alimwambia mamake ameenda kukutana na mwanamuziki.

Muhtasari

•Ripoti iliyoandikishwa katika kituo cha polisi iliashiria kwamba Mwathi alijitoa uhai kwa kuruka chini kupitia dirisha la nyumba ya mwimbaji.

•"Sawa mama, acha niende. Nakaa vizuri. Nitaenda kupiga picha na yeye tukipatana na yeye," Mwathi alisikika akisema.

Marehemu Geoffrey Mwathi
Image: HISANI

Familia moja inadai haki kufuatia kifo cha kijana mwenye umri wa miaka 23  baada ya kudaiwa kuanguka kutoka ghorofa ya kumi ya nyumba ya msanii maarufu wa nyimbo za Kikuyu katika mtaa wa Kasarani, jijini Nairobi.

Kulingana na ripoti ya Inooro TV, Geoffrey Mwathi Ngugi alipatikana akiwa amefariki mnamo Februari 22 na ripoti iliyoandikishwa katika kituo cha polisi iliashiria kwamba alijitoa uhai kwa kuruka  kupitia dirisha la nyumba ya mwimbaji mashuhuri wa Mugithi.

Mwathi anaripotiwa kutembelea nyumba ya mwimbaji huyo baada ya kumtafuta ili amsaidie katika kurembesha duka lake. Baada ya kupata kazi hiyo, kijana huyo aliwasiliana na mama yake anayeishi nchini Qatar ili kumpa habari hizo njema na kumuomba nauli ya kufika hadi ambapo walikuwa wakutane.

"Mama, aki tafadhali si unitumie mia mbili saa hii. Nimepigiwa na ++, ameniambia niende tupatane na yeye hapa Ruiru saa hii. Alafu sikuwa na pesa, nilikuwa nangoja pesa jioni," Mwathi alimwambia mamake. 

Mamake marehemu pia alifichua ujumbe ambao alimtumia kwenye WhatsApp wakati akielekea kukutana na mwimbaji huyo.

"Sawa mama, acha niende. Nakaa vizuri. Nitaenda kupiga picha na yeye tukipatana na yeye," alisikika akisema.

Baada ya kukutana na mwimbaji huyo, marehemu alimwarifu mamake kuhusu kazi ambayo mwimbaji huyo alitaka amfanyie na akamweleza kuwa ingemletea fedha nzuri ambazo yeye na nduguye wangetumia kununua mavazi.

Kulingana na ripoti ya polisi, baadae Mwathi aliandamana na mwanamuziki huyo kwenda katika maeneo manne ya burudani. Picha za CCTV zilionyesha wakirejea nyumbani kwa msanii huyo usiku wa kuamkia tarehe 22 Februari.

Akizungumza na Inooro TV, mjomba wa Mwathi alisema mwimbaji huyo baadaye kidogo aliondoka na kumwacha marehemu pamoja na wanaume wawili ambao pia waliondoka baada ya muda. Alisema wawili hao hawakuenda mbali na walirudi ndani ya nyumba dakika chache kabla ya Mwathi kuonekana akianguka.

Mwanafamilia huyo pia alidai kwamba suruali ya Mwathi ilikuwa imeteremka hadi chini wakati alipoanguka ila uchunguzi wa maiti haukuweza kubainisha ikiwa marehemu alidhulumiwa kingono kabla ya kufariki.

Baada ya kurudi nyumbani na kuona mwili wa Mwathi ukiwa umelala chini, msanii huyo na wenzake waliandamana hadi kituo cha polisi ambapo waliandikisha ripoti kuwa marehemu aliruka chini kupitia kwa dirisha bila ufahamu wa waliokuwa ndani. Waliandika kuwa marehemu alikuwa na mawazo ya kujitoa uhai.

Familia ya Mwathi hata hivyo imetupilia mbali madai kwamba alikuwa na mawazo ya kujitoa uhai huku sasa wakidai majibu.

Juhudi za Radio Jambo kumfikia mwanamuziki huyo na meneja wake ziligonga mwamba kwani simu zetu hazikuchukuliwa.