Waigizaji wawili warembo wa Bongo ambao kwa nyakati tofauti waliwahi kuwa na mahusiano na mwimbaji Harmonize, Frida Kajala Masanja na Jacqueline Wolper wamedhihirisha wazi kuwa wana uhusiano mzuri.
Siku ya Jumapili, walishiriki muda pamoja katika hafla waliyohudhuria na walionyesha picha na video zao wakiwa pamoja.
Katika moja ya video alizochapisha Kajala, wawili hao walionekana wakiburudika pamoja huku wakicheza wimbo wa Whozu na Marioo 'VAVAYO.' Wote walikaa kwenye meza moja wakitingisha miili yao kwa furaha.
Wolper ambaye ni mke wa mfanyibiashara Rich Mavoko alikuwa mpenzi wa kwanza mashuhuri aliyejulikana wa Harmonize. Wawili hao walijitosa kwenye mahusiano mwaka wa 2016 kabla ya kuachana mwezi Februari 2017.
Katika mahojiano ya awali, Wolper alisema kutengana kwake na bosi huyo wa Kondegang ni kwa jinsi alivyopenda pesa.
"Bado Harmonize anatafuta maisha, mimi ni mrembo na nimetafutwa sana na wale wenye kuniwezesha. Kwa upande wangu nilishindwa kutekwa na wenye pesa, kumbe mwenzangu hakua hivyo," aliambia Mpasho.
Mama huyo wa watoto wawili alisema alikuwa na uhakika kuwa mwimbaji huyo bado alimpenda sana licha ya kuachana.
"Sio kwamba alikua hanipendi lakini yeye alikua ni msanii mdogo kwangu, akatokea mtua anaeza kusaidia zaidi ya Wolper akaona kule ndio fursa zaidi.Pesa ilizidi nguvu kuliko penzi," alisema Wolper.
Harmonize alijitosa kwenye mahusiano na Kajala mwaka wa 2021 kabla ya kutengana kisha kurudiana tena mwaka jana. Wawili hao walirudiana Mei mwaka jana baada ya Kajala kukubali kumsamehe mwimbaji huyo.
Hata hivyo, mahusiano yao hayakudumu kwani mwishoni mwa mwaka jana Kajala alitangaza kwamba wametengana.
Wakati akitangaza kutengana na Harmonize mwishoni mwa mwaka jana, Kajala aliweka wazi kwamba alikuwa tayari kupiga hatua nyingine baada ya mahusiano yao ya miezi michache kugonga mwamba.
Ingawa hakufichua kilichowatenganisha, aliweka wazi kwamba hakubeba kinyongo chochote dhidi ya mwimbaji huyo.
"Mimi kama mwanamke na binadamu nimeumbwa kupenda na kusamehe pia, ila kwenye hili nastahili kuchekwa, nastahili kubezwa na kudharauliwa pia. Sipo hapa kujitetea wala kutia huruma ni kweli nilifanya makosa na nimeyagundua makosa yangu, mimi siyo mkamilifu," Kajala alisema mwezi Desemba.