Limousine, Karamu; Sonko atoa zawadi nono kwa Omanyala baada ya kushinda dhahabu

Sonko ameomba serikali kumruhusu amuandalie Omanyala mapokezi mazuri na sherehe kubwa atakapokuwa akirejea nchini.

Muhtasari

• Omanyala aliishindia Kenya dhahabu ya kwanza kabisa katika mbio za mita 100 kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola.

•Sonko pia alimhakikishia Omanyala kuhusu upendo mkubwa wa Wakenya kwake kwa kuleta utukufu nyumbani na kutufanya tujivunie.

Image: FACEBOOK// MIKE SONKO

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko amedokeza kuhusu mpango wake wa kumzawadia mwanariadha Ferdinand Omanyala na gari aina ya Limousine baada ya kutwaa dhahabu kwenye mashindano ya Jumuiya ya madola yanayoendelea jijini Birmingham, Uingereza.

Jumatano usiku Omanyala aliishindia Kenya dhahabu ya kwanza kabisa katika mbio za mita 100 kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola  alipoibuka  wa kwanza baada ya kukimbia kwa sekunde 10.02.

Sonko ni mmoja wa waliompongeza Omanyala huku akiiomba serikali ya Kenya kumruhusu amuandalie bingwa huyo wa Afrika katika mbio za mita 100 mapokezi mazuri na sherehe kubwa  atakapokuwa akirejea nchini.

"Mlipokuwa mmelala mnaota Mkenya mmoja ambaye ni  mwanaume mwenye mbio kubwa zaidi Afrika nzima Ferdinand Omanyala ameshindia nchi ya Kenya dhahabu kwenye Commonwealth Games, akiandikisha sekunde 10.02. Pongezi sana na serikali ikikubali nitakupangia sherehe kubwa ya kukuaki na limousines 15 zikupokee na nikufanyie shereye ya 10 days na nikupee limo moja bure iwe yako," Sonko alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Mwanasiasa huyo pia alimhakikishia Omanyala kuhusu upendo mkubwa wa Wakenya kwake kwa kuleta utukufu nyumbani na kutufanya tujivunie.

Omanyala akisherehekea ushindi wake baada ya kutwaa dhahabu aliwashukuru wote waliounga mkono azma yake ya kupata ubingwa.

Isaya 55.5 , Kwa utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Asanteni sana kwa uungwaji mkono na motisha," Omanyala alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Aliongeza "BINGWA WA AFRIKA sasa ndiye BINGWA WA JUMUIYA YA MADOLA!"

Maelfu ya Wakenya wakiwemo viongozi na watu maarufu  wameendelea kumpongeza bingwa huyo wa mbio za mita 100  kupitia mitandao ya kijamii.