logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Majonzi huku aliyefariki katika ajali iliyohusisha msanii wa Marioo akizikwa, hali ya majeruhi yafichuliwa

Abbah Process alifichua baadhi ya maelezo kuhusu marehemu akisema alikuwa hasa katika idara ya uchukuzi.

image
na Radio Jambo

Habari13 November 2023 - 09:26

Muhtasari


•Marioo, Chino Kidd, Producer Abbah miongoni mwa wengine walihudhuria ibada ya mazishi ya mwenzao Nabeel Jumapili alasiri.

•Abbah Process alifichua baadhi ya maelezo kuhusu marehemu akisema alikuwa hasa katika idara ya uchukuzi.

Mastaa wa Bongo Marioo, Chino Kidd, Loui, Producer Abbah Process miongoni mwa wengine mnamo Jumapili alasiri walihudhuria ibada ya mazishi ya mwenzao Nabeel ambaye alifariki kufuatia ajali mbaya Jumamosi.

Nabeel aliripotiwa kufariki Jumapili asubuhi kufuatia majeraha mabaya aliyoyapata baada ya kuhusika kwenye ajali mbaya ya barabarani katika eneo la Kabuku, mkoa wa Tanga. Marehemu alikuwa akiendesha gari lililokuwa limembeba msanii Chino Kidd na wenzake wengine wakati tukio hilo la bahati mbaya lilifanyika.

Picha na video za mazishi hayo yaliyofanyika katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam siku ya Jumamosi zinaonyesha waombolezaji wakiwa wamegubikwa na hisia kali za majonzi wakati wa kumuaga kijana huyo.

Chino Kidd ambaye alinusurika kwenye ajali hiyo mbaya ya barabarani alionekana akibubujikwa na machozi baada ya mwili wa marehemu kuzikwa na waombolezaji wengine wakajitolea kumfariji. Alionekana kuwa na majeraha usoni mwake ambayo kuna uwezekano mkubwa alipata kutokana na ajali hiyo.

Bosi wa Bad Nation, Marioo kwa upande wake alionekana kuwa na uso wenye huzuni tele na alifunika kichwa chake wakati wote wa mazishi.

Baada ya mazishi, mtayarishaji Abbah Process alifichua baadhi ya maelezo kuhusu marehemu akisema alikuwa hasa katika idara ya uchukuzi.

Aidha alifichua kuwa baadhi ya wachezaji densi waliojeruhiwa vibaya katika ajali hiyo wanaendelea na matibabu maalum katika hospitali.

“Majeruhi wote wapo hospitalini. Hawajaruhusiwa kuondoka, wote bado wako hospitali na wameshindwa kuhudhuria,” alisema.

Producer Abbah alisema mwimbaji Chino Kidd ndiye aliyejeruhiwa kidogo zaidi katika ajali hiyo kwani waathiriwa wengine walikuwa wamejeruhiwa vibaya na kuvunjika baadhi ya sehemu za mwili.

Marehemu Nabeel alifariki kufuatia ajali mbaya iliyotoea siku ya Jumamosi ambayo ilimhusisha msanii Chino Kidd na kundi lake la muziki.

Chino Kidd na wenzake kadhaa walikuwa wakielekea katika mkoa wa Tanga kwa ajili ya shoo wakati gari aina ya Alphard nyeusi walilokuwa wamepanda, na ambalo liliendeshwa na Nabeel liligongana na lori la mafuta ya petroli.

Ajali hiyo inaripotiwa kutokea katika eneo la Kabuku Jumamosi mchana ambapo waathiriwa kadhaa wanaripotiwa kupata majeraha mabaya.

Mtayarishaji wa muziki kutoka Tanzania Abbah Process alithibitisha kifo cha Nabeel Jumapili asubuhi alipokuwa akimuomboleza.

“Rest in peace brother, tumepoteza mwanafamilia mmoja aliyekuwa kwenye ajali ya jana (Jumamosi). Mungu amkumbatie katika mikono yake yenye upendo na ampe amani ya milele. Milele mioyoni mwetu,” Abbah Process aliandika kwenye akaunti yake ya Instagram.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved