Makiwa! Mwanamuziki Stivo Simple Boy ampoteza baba yake

Stivo Simple Boy yuko katika majonzi baada ya kumpoteza baba yake Anthony Adera.

Muhtasari

•"Ni kwa majuto na huzuni kwamba tunatangaza kifo cha Anthony Adera, baba yake Stephen Otieno Adera anayejulikana kama Stevo Simple Boy," sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.

•Mwanamuziki huyo ni mzaliwa wa saba katika familia ya watoto wanane.

Image: INSTAGRAM// STIVO SIMPLE BOY

Mwimbaji Stephen Otieno Adera almaarufu Stivo Simple Boy yuko katika majonzi baada ya kumpoteza baba yake Anthony Adera.

Habari kuhusu kifo cha Bw Adera zilitangazwa kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa  Instagram wa Simple Boy siku ya Jumapili asubuhi na lebo yake ya muziki ya Men in Business (MIB)

"Ni kwa majuto na huzuni kwamba tunatangaza kifo cha Anthony Adera, baba yake Stephen Otieno Adera anayejulikana kama Stevo Simple Boy," sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.

MIB walitoa wito kwa mashabiki wa msanii huyokutoka Kibra kusimama naye kwa maombi katika kipindi hiki kigumu cha maisha yake.

“Taarifa zaidi zitawasilishwa,” taarifa ilisoma.

Wazazi wa Stivo wanatokea Oyugis katika Kaunti ya Homabay ambapo mwanamuziki huyo wa nyimbo za kufoka alizaliwa na kukulia kabla ya kuhamia jijini Nairobi baada ya kumaliza elimu ya Shule ya Msingi.

Mwezi Julai mwaka jana, msanii huyo alifichua kuwa aliwajengea wazazi wake nyumba kijijini hapo baada ya shoo na dili zilizofanikiwa.

Alifichua kuwa aliwajenga  wazazi wake  kwa kutumia pesa alizopokea alipokuwa akifanya kazi na usimamizi wake wa zamani.

“Nilipokea nusu milioni katika tangazo la dau la Odi. Nilitumia pesa hizo kuwajengea wazazi wangu nyumba,” Stivo Simple Boy alisema.

Mwanamuziki huyo ni mzaliwa wa saba katika familia ya watoto wanane.