"Mamangu akifa sitahisi chochote!" Mtumishi afunguka uganga wa mamake ulivyoleta taabu katika familia yao

Mtumishi alisema kuwa ana uchungu sana na mama yake mzazi na akabainisha kuwa hata akifa leo, hawezi kumuomboleza

Muhtasari

•Mtumishi alidai kuwa mama yake amekuwa akishiriki uchawi kwa miaka mingi, kitu ambacho alitumia kuvunja familia yake.

•“Nakumbuka tukiwa ushago kwa shosh, mama yangu aliniambia sitapata amani hadi nife, nilikuwa mtoto mdogo,” alisema.

Mchekeshaji Gilbert Barasa almaarufu Mtumishi
Image: HISANI

Aliyekuwa mchekeshaji  wa Churchill Show, Gilbert Barasa almaarufu Mtumishi amemshutumu mama yake mzazi kwa kuvunja familia yake na kumkana waziwazi.

Wakati akizungumza katika ibada ya kanisa la Jesus Compassion Ministry siku ya Jumapili, Mtumishi alidai kuwa mama yake amekuwa akishiriki uchawi kwa miaka mingi, kitu ambacho alitumia kuvunja familia yake.

Mchekeshaji huyo alifunguka kuhusu jinsi mamake alivyomhusisha katika shughuli zake za uchawi dhidi ya baba yao akibainisha kuwa mwanamke huyo aliyemzaa hakuwa sahihi kufanya hivyo.

“Mama yangu alivunja boma lake. Kwa nini niseme hivi, alinihusisha kwa mambo ambayo mimi sifai kuhusika. Nikiwa mdogo alikuwa ananipatia dawa za waganga niekee baba yangu kwa mlango ili akija afanye nini… Bila shaka, kila mara mtoto ana hisia na hana hatia , baba yangu akikuja nilikuwa namwambia mama alinipea niweke kitu hapa alafu anatoa inakuwa ni vita kwa nyumba,” Mtumishi aliwaambia washirika.

Mtumishi alieleza kuwa muda wote huo yeye hakuwa na hatia kwani katika umri wake, hakujua mama yake alikuwa akimhusisha katika nini.

Alifichua kwamba hatimaye wazazi wake walitengana na mama yake akaenda katika ofisi za FIDA ambapo aliruhusiwa kuchumasehemu ya mshahara wa baba yake.

"Mama yangu hakuwahi acha uganga, aliharibu familia yake kabisa, akaharibu ndoa yake kabisa," Mtumishi alisema.

Mchekeshaji huyo alisema kuwa baadaye maishani alipata kuzungumza na baba yake ambapo mzazi huyo alimweleza kuwa alilazimika kumuacha mama yao kwa sababu ya uchawi wake.

Aidha, alifichua kuwa mama yake hakuwahi kumuunga mkono alipokuwa akianza kazi yake ya ucheshi katika Churchill Show miaka mingi iliyopita na hata alimkana kutokana na usanii wake na kumfukuza nyumbani kwake.

Mtumishi alifungukakuwa mama yake pia hakuwahi kumtaka aliyekuwa mkewe na akadai kuwa hata alitumia uchawi kuvunja ndoa yao miezi minne tu baada ya harusi.

"Tangu 2021, sijazungumza na mama yangu baada ya tukio hilo, sina furaha kumuona mama yangu," alisema.

Mchekeshaji huyo alisema kuwa ana uchungu sana na mama yake na kubainisha kuwa hata akifa leo, hawezi kumuomboleza kabisa.

“Mimi mama yangu, acha tu niseme ukweli, hata akifa leo, sitahisi chochote. Kwa miaka miwili iliyopita, tangu 2021, sijaongea na yeye,” alisema.

Mtumishi alifichua kuwa tangu mama yake kudaiwa kuvunja ndoa yake mwaka 2021, amekuwa akipuuza simu zake kwani hayuko tayari kuzungumza naye.