'Babangu alisema nilitoshana na panya!' King Kaka afunguka kuhusu kuzaliwa kwake kabla ya wakati

Muhtasari

•King Kaka alieleza kwamba kilichosababisha mamake kujifungua mapema ni mshtuko uliompata baada ya kupokea taarifa kuwa mwanawe mkubwa alikuwa ameanguka kutoka kwa mti.

Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Mwanamuziki mashuhuri wa nyimbo za kufoka Kennedy Ombima almaarufu kama King Kaka amefunguka kuhusu utoto wake na utata uliozingira kuzaliwa kwake.

Akiwa kwenye mazungumzo na Mwafrika katika kipindi cha 'Iko nini', King Kaka alifichua kwamba alizaliwa miezi miwili kabla ya wakati wa mamake kujifungua kutimia.

King Kaka alieleza kwamba kilichosababisha mamake kujifungua mapema ni mshtuko uliompata baada ya kupokea taarifa kuwa mwanawe mkubwa alikuwa ameanguka kutoka kwa mti.

"Nilizaliwa Bahati. Kakangu mkubwa alianguka kutoka kwa mti. Kwa wakati huo mamangu alikuwa mjamzito. Mama alikuwa ametulia kwa nyumba na ujauzito wake watoto wakaja wakamwambia Kevo ameanguka kutoka kwa mti. Mama alikuwa na ujauzito wa miezi saba, akapata mshtuko ikabidi nimetoka" King Kaka alisimulia.

King Kaka alisema kwamba baada ya mamake kupatwa na mshtuko alikimbizwa hospitalini ambapo madaktari walimwarifu kuwa kulikuwa na uwezekano wa yeye au mtoto kupoteza maisha.

Hata hivyo aliweza kujifungua ila rapa huyo akazaliwa akiwa na mwili mdogo zaidi kuliko kawaida.

"Nikizaliwa mbuyu alikuwa anasema nilikuwa natoshana kama panya. Wauguzi walikuwa wanaambia mamangu ni aidha yeye aage ama mtoto. Kushangaza zaidi sote tulikuwa sawa" Kaka alisema.

Mwanamuziki huyo pia alifichua kwamba alimpoteza babake kutokana na ugonjwa wa mapafu akiwa katika darasa la saba.