Billnass amvisha Nandy pete ya Uchumba, ndoa mwezi wa 6

Muhtasari

• Msanii Billnass amemvisha pete ya uchumba mchumba wake wa muda mrefu ambaye pia ni msanii wa kizazi kipya, Nandy mbele ya wazazi wake na kulipa mahari ya kima cha milioni kumi za Kitanzania mnamo Februari 20

Billnass na Nandy
Image: Nandy (Facebook)

Msanii Billnass amemvisha pete ya uchumba mchumba wake wa muda mrefu ambaye pia ni msanii wa kizazi kipya, Nandy mbele ya wazazi wake na kulipa mahari ya kima cha milioni kumi za Kitanzania mnamo Februari 20.

Wawili hao wamekuwa kwenye mahusiano kwa muda mrefu sana na mahusiano yao yalikuwa yamejulikana sana mitandaoni na kwa mashabiki lakini siku ya jana ndio rasmi walitambulishana kwa wazazi na marafiki walioalikwa nyumbani kwao Nandy.

Kwenye mkanda wa video uliosambazwa mitandaoni, Billnass anaonekana akipiga magoti chini na kumvisha pete Nandy ambapo inaarifiwa ametoa mahari ya milioni 10 za Kitanzania na pete yenyewe inatajwa kuwa ya thamani ya milioni 8 za Kitanzania. Ina maana kwamba Billnass ametumia kiasi cha milioni 18 za Kitanzania nyumbani kwake Nandy.

Billnass hakuenda kinyonge kabisa kwani aliongozwa na msafara wa magari makubwa kweli na Rafiki zake ambapo walitua nyumbani kwa kina Nandy na kupokelewa kwa shangwe kubwa kwa shughuli kubwa ya kuonana na wakwe zake kwa mara ya kwanza na kufanya taratibu zingine za kimila

Akizungumza baada ya tukio hilo, Nandy amewahakikishia mashabiki na wafuasi wake kwamba sasa watarajie ndoa na Billnass baada ya taratibu za mila kukamilika hiyo jana.

“Ni siku yenye baraka sana kwenye familia yangu na familia ya mume wangu mtarajiwa. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kulitimiza hili salama, na tuseme tu ni hatua kubwa, tunamuomba Mungu ili tuweze kulitimiza mbeleni Zaidi,” alisema Nandy.

Vule vile Nandy alifichua kwamba sasa rasmi mazungumzo ya ndoa yameng'oa nanga na ndoa yenyewe haiwezi ikapita mwezi wa sita wa mwaka huu 2022.

Kila la kheri Nandy na Billnass!