Matumizi yangu ya wiki ni kiasi cha milioni moja - Noti Flow

Muhtasari

• Msanii tokea nchini Kenya, Natalia Florence almaarufu Noti Flow amewashangaza wengi baada ya kufichua kwamba yeye hutumia takribani milioni moja, pesa za Kenya, kwa wiki

• Pia amewaonya wanaofurika kwenye DM yake kwamba yuko katika mahusiano yenye furaha na mpenzi wake King Alami

Noti Flow
Image: Facebook

Msanii tokea nchini Kenya, Natalia Florence almaarufu Noti Flow amewashangaza wengi baada ya kufichua kwamba yeye hutumia takribani milioni moja, pesa za Kenya, kwa wiki katika mambo yake.

Unapozungumzia umaskini na uhaba wa pesa, bila shaka kwa Noti Flow ni kama hekaya za abunuwasi kwani yeye ananukia ukwasi.

Noti Flow alipata kuyafichua haya baada ya kughadhabishwa na mtu katika ukurasa wake wa Instagram aliyetaka kumpa laki mbili pesa za Kenya ili wawe katika mahusiano ya muda mfupi ya mahanjumati naye na hapo ndipo alimpasha na kusema kwamba laki mbili kwake si kitu kwani katika wiki ambayo hajihisi kutumia pesa kabisa basi hutumia nusu milioni, na wiki ambayo ako katika ubora wa matumizi yake basi ni milioni kwenda mbele.

“Manigga kama hawa wanafanya najihisi mgonjwa. Muda wote wamekita kambi kwenye DM yangu wakidhani wataninunua na pesa kidogo hivi,” aliandika Noti Flow

Hapo ndipo aliendelea kuelezea jinsi yeye hufanya matumizi yake.

“Kwa wiki mimi hutumia $4500 za Kenya na hiyo ni wiki ambayo niko mvivu kwa matumizi. Kwa kawaida huwa natumia $10,000 kwa wiki wakati nina mtoko. Tuliza makorodani yako na ujichunguze,” alimpasha mwanaume huyo.

Mwanamuziki huyo alizidi kuelezea kwamba yuko Katika mahusiano ya kimapenzi yenye furaha Zaidi na mpenzi wake King Alami, mahusiano ambayo wawili hao waliyaweka bayana mwaka jana.

“Niko na furaha sana katika mahusiano yangu na mrembo wangu. Sihitaji vipesa vyako hivyo ambavyo kwangu ni kama salio tu. Na hili linaenda pia kwa wavulana na wasichana wote mnaojaza DM yangu. Sina peremende za kuwapa mimi,” aliandika Noti Flow

Je, wewe kwa wiki matumizi yako ni ya thamani ya kiasi kipi?