Hospitali ya Muhimbili yakana kurekodi video ya prof. Jay

Muhtasari

• Hospitali ya Taifa Muhimbili imekana madai kwamba ilihusika katika kusambaza video za Professor Jay akiwa hospitalini.

• "Uongozi wa hospitali unatoa taarifa kuwa video hii haijarekodiwa na kusambazwa na hospitali, tumesikitishwa na tunalaani vikali kitendo hiki cha kumrekodi mgonjwa,” hospitali hiyo ilisema katika taarifa.

 

Mwanamuziki Joseph Haule almaarufu kama Profesa Jay
Mwanamuziki Joseph Haule almaarufu kama Profesa Jay
Image: HISANI

Hospitali ya Taifa Muhimbili imekana madai kwamba ilihusika katika kusambaza video za Professor Jay akiwa hospitalini.

Usimamizi wa hospitali hiyo ulilazimika kutoa taarifa hiyo baada ya video kuonekana na kusambazwa kupitia ukurasa wa mwanaharakati Mange Kimambi, ikionyesha Professor Jay akipewa matibabu hospitalini humo.

"Uongozi wa hospitali unatoa taarifa kuwa video hii haijarekodiwa na kusambazwa na hospitali, tumesikitishwa na tunalaani vikali kitendo hiki cha kumrekodi mgonjwa,” hospitali hiyo ilisema katika taarifa.

Kulingana nao sio haki kumrekodi mgonjwa bila idhini yake hasahsa anapopigania uhai wake katika ICU, wakitaja kitendo hicho kama kukosa maadili na utu.

  "Tunafuatilia kwa ukaribu tukio hili ili kubaini chanzo cha video hiyo ili hatua stahiki zichukuliwe.Wananchi endeleeni kuwa na imani na Hospitali ta Muhimbili," imeeleza taarifa iliyotolewa na Hospitali ya Muhimbili.

Ifahamike kwamba msanii huyo amekuwa akipokea matibabu kwa muda mrefu sasa huku familia yake ikitarajiwa katika wakati faafu kutoa taarifa kuhusu chanzo chake kulazwa.