'Luku' ya nusu uchi ya Iyanii iligharimu kiasi cha Ksh 300,000

Muhtasari

• Msanii Iyani aliingia jukwaani nusu uchi lakini Arrow Bwoy amefichua kwamba muonekano ule uligharimu laki tatu za Kenya.

msanii wa kizazi kipya Iyanii
msanii wa kizazi kipya Iyanii
Image: Instagram

 Juzi katika uzinduzi wa albamu kwa jina Focus yake msanii Arrow Bwoy, palitokea vioja vingi tu ambavyo viliwashangaza wengi katika hafla hiyo, ambapo pia Arrow Bwoy hatimaye alimvisha pete ya uchumba mpenzi wake Nadia.

Moja kati ya matukio makubwa yaliyowaacha wengi wakiwa macho kodo na midomo wazi ni muonekano wa msanii Iyanii ambaye ni chipukizi.

Katika hafla ya uzinduzi wa albamu hiyo, Iyanii alitokea jukwaani akiwa amevalia nusu uchi kama kinyago vile na kuibua hisia mseto na kinzani kwenye mitandao ya kijamii.

Arrow Bwoy ambaye ni kama baba ya Iyanii katika Sanaa ya muziki chini ya kundi la Utembe hatimaye amejitokeza wazi na kumtetea Iyanii kwa muonekano wake wa kustaajabisha.

Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha redio wakati wa ‘media tour’ yake ili kusambaza albamu yake, Arrow Bwoy alimtetea Iyanii na kusema kwamba ile ni fasheni tu ambayo pia walikuwa wanatangaza kazi ya mmoja wao katika kundi la Utembe anayejitafutia riziki kupitia fasheni.

Aidha, Arrow Bwoy aliweka wazi kwamba hata kama watu walimchamba Iyanii kwa muonekano wa kasoro uchi, muonekano wenyewe ulikuwa umewagharimu kiasi kikubwa sana cha pesa mpaka kumfanya atokee vile.

Alisema muonekano wenyewe ulipiga kiasi cha laki tatu taslimu za Kenya na kuwataka Wakenya waache kuangalia tu upande hasi wa kila matukio kwa sababu ile ilikuwa ni fasheni tu na ambayo iligharimu kiasi kikubwa zaidi ya maelezo.

Je, unakubaliana na Arrow Bwoy kwamba muonekano wa Iyanii katika hafla ya uzinduzi wa albamu ya Focus uligharimu kiasi cha elfu 300 za Kenya?