Erick Omondi amsifia Edgar Obare kwa 'kuwaanika' wasanii

Muhtasari

• Erick Omondi alisema kwamba anaunga mkono michakato ya mwanablogu Edgar Obare kuendelea 'kuwaanika' wasanii.

• Aliongezea kwamba kwa kiasi fulani mashabiki wanapaswa kufahamu hali ya maisha ya wasanii hao.

Eric Omondi
Eric Omondi
Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mcheshi Erick Omondi kwa mara ya kwanza amempongeza mwanablogu Edgar Obare kwa harakati zake za kufichua siri za wasanii wengi humu nchini.

Akizungumza katika mahojiano na Spm Buzz, Omondi alisema kwamba Obare anapaswa kulipwa na kupewa heshima kwa kuwa amelisaidia gemu la burudani.

Omondi alishikilia kwamba mwanablogu huyo amesaidia pakubwa katika kuchangamsha sanaa, na kumtaka aendelea na juhudi hizo.

"Edgar amekuwa mtu wa maana katika sanaa yetu, anapaswa kupewa heshima yake," Erick Omondi alisema.

Vilevile alisema kwamba mtu anapokuwa maarufu, basi kwa kiasi fulani mashabiki wanatakiwa kujua kinachoendelea katika maisha yake.

Aliwataka wasanii kutompiga vita Obare na badala yake kumpa sapoti ili sekta ya burudani izidi kufana.

Ifahamike kwamba Obare kwa muda mrefu sasa, amekuwa akiweka wazi kwa umma siri za wasanii jambo ambalo kwa mara kadhaa limempelekea kujikuta matatani.