Mcheshi na mwanablogu, Vinnie Baite ameweka wazi sababu yake ya kuamua kuzamia kazi za mitandao badala kuajiriwa.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha Clouds fm huko Tanzania, Baite alisema kwamba alikosa kazi baada ya kumaliza masomo yake ya chuo kikuu, hivyo kulazimika kutafuta mbinu mbadala ya kupata hela.
Baite alishikilia kwamba ucheshi na uanablogu unapaswa kuchukuliwa kama kazi zingine rasmi kwa kuwa zimefanikiwa kutoa nafasi za ajira kwa vijana wengi.
"...Nilijua kupata kazi sio rahisi, kwa hiyo nikaamua kujiajiri mwenyewe," Baite alisema.
Kulingana naye, hajuti kabisa kuwa mwanablogu kwa sababu kazi hiyo imempa maisha ambayo angetamani kuwa nayo, na anazidi kupaa katika viwango vya juu.
Aliongezea kwamba kwa sasa ana lengo la kukuza mitandao yake ya kijamii na kupata wafuasi wengi ili kuongeza ushawishi wake wa kibiashara.
Mcheshi huyo pia hakukosa kuwashukuru wale wote ambao wamempa sapoti tangu anaanza mpaka alipofikia.
Aliwaahidi mashabiki wake kwamba atazidi kutoa kazi nzuri na za kuburudisha.