Omosh wa Tahidi High ajutia kuingia katika ulevi

Muhtasari

• Muigizaji huyo alisema anajutia kujitosa katika utumiaji wa vileo.

• Alisema kwa sasa anazingatia kuboresha maisha ya familia yake.

Muigizaji Omosh amesema kwamba anajutia kujitosa katika ulevi, jambo ambalo kwa asilimia kubwa lilichangia maisha yake kuporomoka.

Akizungumza katika mahojiano na mwanablogu mmoja nchini, Omosh alisema kwamba alitumia pesa nyingi kwa pombe na anahisi kwamba angezitumia kuboresha  hali ya maisha yake.

Alisema kwamba uraibu wa pombe ni ugonjwa, na watumizi wengi wanatamani kuacha kwa sababu wanapoteza hela nyingi kwa mambo yasiyo ya maana.

"...Ulizia watu wengi wanaokunywa, unaeza ona wako na furaha ila wanatamani kuacha," Omosh alisema.

Omosh alishikilia kwamba ulevi ndo ulimpelekea kukosa kuwekeza na kufanya maisha yake yawe magumu asijue pa kukimbilia.

Alidokeza kwamba tayari amesharejelea kazi yake ya uigizaji katika kipindi cha Tahidi High, na sasa maisha yake yanaanza kunyooka.

Hakusita kumshukuru mkewe kwa kumpa sapoti kipindi alikuwa anapitia changamoto za kimaisha.

Amewaahidi mashabiki zake kuzidi kumfuatilia kwa kuwa ana kazi nyingi ambazo amezipanga.