Nadia amkemea vikali promota aliyemlazimisha kutumbuiza siku 3 tu baada ya kupoteza mimba

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 25 amesema alikosa kumaliza shoo hiyo kwa kuwa alilemewa.

•Amefichua kwamba kwa wakati huo alikuwa anapitia kipindi kigumu baada ya kupoteza mimba mapema wiki hiyo.

Image: INSTAGRAM// NADIA MUKAMI

Mwezi Mei mwaka jana, mwanamuziki Nadia Mukami alikejeliwa na kukosolewa sana mitandaoni kwa kukosa kumaliza kutumbuiza katika tamasha yake mjini Busia.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 25 amesema alikosa kumaliza shoo hiyo kwa kuwa alilemewa.

Nadia ambaye alijifungua mtoto wa kiume hivi majuzi amefichua kwamba kwa wakati huo alikuwa anapitia kipindi kigumu baada ya kupoteza mimba mapema wiki hiyo.

"Kuna promoter wa Busia alikuwa amelipa pesa kiasi kitambo. Hapo awali singeweza kutumbuiza kwa sababu ya lockdown. Baada ya lockdown kuondolewa sasa ningeweza kutumbuiza. Nilitoka hospitali siku ya Jumatano alafu akasisitiza lazima nitumbuize Jumamosi hiyo," Nadia alisimulia kwenye mtandao wa Youtube.

Mwanamuziki huyo alidai kwamba waandalizi wa tamasha hiyo walimuweka katika mazingira hafifu na walimtendea vibaya.

Alisema wakati alipoalikwa jukwaani aliweza kutumbuiza kwa nusu saa tu ila akashindwa kuendelea. Alieleza kwamba promota alitaka aendelee kutumbuiza kwa lazima.

"Nilikuwa siwezi kusonga sana kwa kuwa nilikuwa nimetoka hospitalini. Aliita wahuni wake akasema siwezi kutumbuiza kwa dakika 30 nirudi kwenye jukwaa. Kidogo tupigane," Alisimulia.

Mume wake, Arrow Bwoy alisema tukio hilo lilimvunja moyo sana nusura aende kukabiliana na promota huyo.