Nadia Mukami abubujikwa na machozi akisimulia huzuni iliyomkumba baada ya kupoteza mimba

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 25 aliwezwa na hisia alipokuwa anafunguka yaliyojiri wakati ujauzito wake uliharibika.

•Katika kipindi hicho, mama huyo wa mtoto mmoja alijaribu sana kuficha hisia zake na kujifanya kama kwamba yupo sawa.

Image: INSTAGRAM// NADIA MUKAMI

Malkia wa muziki wa kisasa, Nadia Mukami amefichua kwamba alipoteza ujauzito wake wa kwanza mnamo Aprili 12, 2021.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 25 aliwezwa na hisia alipokuwa anafunguka yaliyojiri kupitia Youtube Channel yake.

Nadia alifichua kwamba alikumbwa na kiwewe kikubwa kutokana na tukio hilo la kutisha  hadi kulazimika kupata ushauri wa kisaikolojia.

"Ulikuwa wakati mgumu kuwahi pitia. Huo ndio wakati nilitamani singekuwa msanii. Hospitalini nilioshwa, nilipotoka bado nilikuwa na trauma. Nilipitia kiwewe hadi nikaenda kupata ushauri. Nilikuwa naenda kupata ushauri na watu hawakujua, huo ndio wakati nilikuwa natengeneza ofisi yangu. Nilishauriwa sana na ilisaidia sana," Nadia alisimulia.

Katika kipindi hicho, mama huyo wa mtoto mmoja alijaribu sana kuficha hisia zake na kujifanya kama kwamba yupo sawa.

"Kila mtu alikuwa ananiangalia kama kielelezo, hakuna aliyejali matatizo yangu. Hiyo ndio sababu nilijichagua mimi. Nimeamua kuwa mkweli kadri iwezekanavyo. .. nimepigana sana mwaka uliopita. Kama kuna mtu amejua kujiekelea vitu ni mimi. Nilipoteza marafiki wengi 2021 kwa sababu sikuwa na wakati wa kujieleza," Alisema.

Msanii huyo hata hivyo alibahatika kupata ujauzito mwingine takriban miezi miwili baada ya kupoteza ule wa kwanza. Alijifungua mtoto wa kiume mnamo Machi 4.