Vera Sidika asema kitanda cha mwanawe ni Ksh 300,000

Muhtasari

Vera Sidika - Binti yangu analalia kitanda cha Ksh 300,000 kutoka UK, ninatamani sana ningekuwa na maisha kama hayo nikiwa mtoto mchanga

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Mwanasosholaiti Vera Sidika ambaye pia ni mkewe mwanamuziki Brown Mauzo amewakosha wengi mitandaoni baada ya kufichua gharama kubwa ya kitanda cha mwanawe Asia Brown.

Vera aliandika kwenye instastories zake Jumanne na kufichua kwamba kitanda cha mwanawe wala hakijanunuliwa nchini bali kama vitu vingine vingi tu vya matumizi na Asia, kitanda pia kiliagizwa kutoka kwa tafia la mkoloni, kwa maana ya Uingereza.

Vera Sidika alisema kwamba kitanda hicho ni cha gharama ya shilingi laki tatu taslimu pesa za Kenya!

Katika kile kinachoonekana kama kujaribu kulipiza kwa mwanawe kwile alichokoza katika utoto wake, Vera aliandika kwa kusema kwamba anatamani pia yeye angepata maisha ya nyota tano kama hayo anayompa mwanawe Asia.

“Binti yangu analalia kitanda cha Ksh 300,000 kutoka UK, ninatamani sana ningekuwa na maisha kama hayo nikiwa mtoto mchanga. Kweli nimeamini tunafanya bidi maishani ili tuwape watoto wetu maisha mazuri ambayo sisi hatukufanikiwa kuyapata,” aliandika Vera Sidika.

Mwanasosholaiti huyo ambaye wengi wanasema alishastaafu kutoka kuwa mshawishi mitandaoni baada ya kuingia kwenye ndoa alimalizia kwa kuwashukuru kina mama wote wanaotia bidii maishani ili kufanikisha ndoto ya maisha mazuri kwa wanao.

“Ak Mungu awabariki kina mama wote wanaofanya kweli kwa ajili ya wanao,” alimaliza.