Nawaombea sana, pastor T awataka Bahati na Willy Paul kurudi Gospel

Muhtasari

• Pastor T amesema kwamba angependa sana kuona Bahati na Pozze wakirudi katika muziki wa injili.

• Amesema kwamba walikuwa na ufuasi mkubwa ambao ungeweza kubadilisha maisha ya vijana wengi nchini.

Instagram, KWA HISANI
Instagram, KWA HISANI
Image: Pastor T

Mhubiri Mr T amesema kwamba anatamani kuwaona wasanii Bahati na Willy Paul wakirejea kuimba nyimbo za injili.

Mr T alisema kwamba wawili hao walikuwa na ufuasi mkubwa ambao ungeweza kubadilisha ya vijana wengi na kuwaleta kanisani.

Alishikilia kwamba wawili hao walijisahau pindi tu walipoanza kupata umaarufu na wakaanza kuimba miziki ya kidunia.

Mtumishi huyo alidai kwamba anafahamu uhusiano wa Bahati na Mungu na angependa kumuona akitumia kipaji hicho kubadilisha maisha ya wakenya.

Kulingana naye hatua ya Pozze na Bahati kuingia katika muziki wa dunia ilipelekea watu wengi hasahasa vijana chipukizi kupoteza matumaini yao kwa Mungu.

"Hawa jamaa hawajui mahali Mungu angewapeleka. Walipata umaarufu wakaamua kubadilika," Mr T alisema.

Aidha, alisema kwamba atazidi kuwakosoa pale ambapo anahisi kwamba wamekwenda kinyume na matakwa ya Mwenyezi Mungu.

Licha ya kuweka wazi kwamba itakuwa vigumu kwa wawili hao kurejelea viwango vyao vya awali, Mr T alidokeza kwamba kuna uwezekano wa wawili hao kurejea katika muziki wa injili.

Bahati kwa sasa yupo katika harakati za kufanikisha kampeni za kuwania ubunge wa eneo la Mathare, huku akiwa amepiga breki kwa muda uimbaji wake.

Kwa upande wake Willy Paul, anazidi kuachia vibao visivyo vya injili ambavyo vinazidi kufanya vizuri katika chati mbalimbali za burudani.