Diamond Platnumz ajigamba jinsi anavyodekezwa na kipenzi chake

Muhtasari

• Diamond  amedokeza kwamba mpenzi wake mpya anamdekeza ipasavyo  na amezama ndani kabisa katika bahari la mahaba.

Diamond Platnumz
Diamond Platnumz
Image: INSTAGRAM

Staa wa Bongo Naseeb Abdul Juma almaarufu kama Diamond Platnumz amedhihirisha wazi kwamba anayafurahia sana mahusiano yake mapya.

Siku za hivi majuzi mwanamuziki huyo hajakuwa akificha furaha kubwa inayotokana na mahusiano yake na malkia aliyeteka moyo wake ambaye bado hajatambulishwa  wazi.

Kupitia Instastori zake, Diamond  amedokeza kwamba mpenzi wake mpya anamdekeza ipasavyo  na amezama ndani kabisa katika bahari la mahaba.

"Dunia bwana ina mambo ya ajabu. Yaani ghafla unajikuta kwenye upendo ambao haujawahi kuufikiria, unajikuta una furaha na kuridhishwa na kila unachofanyiwa. Kweli kua uyaone," Diamond aliandika.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya msanii huyo kumsherehekea mpenzi wake baada yake kumkabidhi zawadi kochokocho.

Diamond alimsifia sana mpenzi huyo wake kwa makubwa aliyomfanyia huku akionekana kuridhishwa na zawadi alizopokea.

"Kumpata anayekupenda ni jambo moja, ila kumpata atakayekuelewa na kukupa unachotaka ni jambo lingine kabisa," Diamond alisema.

Bosi huyo wa Wasafi alimhakikishia mchumba huyo wake kwamba mapenzi yake kwake ni makubwa mno.