Nadia Mukami azungumzia hali yake mpya ya kuwa mama,afichua idadi ya watoto analenga kupata

Muhtasari

•Mchumba huyo wa Arrow Bwoy hata hivyo alidokeza kuwa suala la kushughulikia mtoto mchanga halijakuwa rahisi  kwake

•Mwanamuziki huyo alifichua kwamba anatazamia kupata watoto wengine wawili ili kufunga ukurasa wa kuzaa.

Image: INSTAGRAM// NADIA MUKAMI

Mwanamuziki Nadia Mukami alishirikisha wafuasi wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye Instagram.

Mashabiki walipata fursa ya kumuuliza mama huyo wa mtoto mmoja maswali kemkem kuhusu maisha yake, ndoa na sanaa.

Katika kipindi hicho, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 25 aliweka wazi kwamba anafurahia hali yake mpya ya kuwa mzazi.

"Ni hisia bora zaidi kuwahi kutokea. Mwingine kabla nitimize 30 nimalizane," Nadia alijibu alipoulizwa jinsi anavyohisi kuwa mama.

Mchumba huyo wa Arrow Bwoy hata hivyo alidokeza kuwa suala la kushughulikia mtoto mchanga halijakuwa rahisi  kwake.

"Safari ya ujauzito ni bora kuliko kushughulikia mtoto mchanga. Eh!! Wamama wapewe allowance na serikali kila mwezi," Alisema.

Nadia aliweka wazi kwamba mchumba wake amekuwa akisaidia sana katika kushughulikia mtoto wao wa mwezi mmoja.

"Nina furaha na nashukuru kuwa yeye ni baby daddy wangu na mchumba. (Arrow Bwoy) Yeye ni baba mzuri. Ameosha mwanawe mara nyingi kuniliko kufikia sasa walahhi," Alisema Nadia.

Mwanamuziki huyo alifichua kwamba anatazamia kupata watoto wengine wawili ili kufunga ukurasa wa kuzaa.