Trio Mio azungumza kuhusu madai ya kupata D katika KCSE

Muhtasari

•Trio Mio ameweka wazi kwamba hajawahi kufanya mtihani wa KCSE kwani bado hajakamilisha masomo yake ya shule ya upili.

•Msanii huyo  amebainisha kuwa yeye ni mwanafunzi katika shule moja ya upili ya bweni nchini Kenya.

Image: INSTAGRAM// TRIO MIO

Mwanamuziki Mario TJ almaarufu Trio Mio ametupitlia mbali madai kuwa alikalia mtihani wa KCSE 2021 na kupata alama D.

Trio Mio ameweka wazi kwamba hajawahi kufanya mtihani wa KCSE kwani bado hajakamilisha masomo yake ya shule ya upili.

"Ni uwongo. Ni uwongo jo. Bado nasoma," Trio Mio alisema akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai.

Punde baada ya matokeo ya KCSE 2021 kutangazwa siku ya Jumamosi kulitokea madai kuwa Trio Mio amepata jumla ya alama D na kuandikisha alama E katika Hisabati na Kemia.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 17 amebainisha kuwa yeye ni mwanafunzi katika shule moja ya upili ya bweni nchini Kenya.

"Mimi nitaenda shule bado. Sisomei nyumbani. Mimi bado ni mwanafunzi wa bweni. Nitafika huko baadae," Mio alisema.

Hapo awali akiwa kwenye mahojiano na Churchill, mwanamuziki huyo alifichua kuwa atakalia mtihani wake wa KCSE mwishoni wa mwaka huu.

Trio Mio alisisitiza kuwa usanii wake haujaathiri masomo yake na kusema kila mara anapokuwa darasani huwa anaangazia masomo pekee.

"Kushughulikia muziki na masomo ni rahisi. Kila wakati mistari ikija huwa naandika vizuri, lakini haijawahi kuja mwalimu akiwa darasani. Hicho ndicho kitu cha maana kunitendekea. Haijawahi kutokea eti nianze kufikiria mambo na muziki mwalimu akiwa darasani" Mio alisema.

Mio ni mmoja wa wasanii wenye umri mdogo zaidi ambao wameitikisa tasnia ya muziki  nchini Kenya.