Hongera! Baha wa machachari na mpenzi wake wabarikiwa na mtoto wa kike

Muhtasari

•Tyler alitangaza kuwa mzaliwa wao wa kwanza ni msichana na kufichua kuwa anashiriki tarehe sawa ya kuzaliwa naye.

Image: INSTAGRAM// TYLER MBAYA

Mwigizaji Tyler Mbaya na mpenzi wake Georgina Njenga wamemkaribisha duniani mtoto wao wa kwanza.

Wawili hao walitangaza habari za kuzaliwa kwa mtoto wao siku ya Jumamosi kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamiii.

Tyler alitangaza kuwa mzaliwa wao wa kwanza ni msichana na kufichua kuwa anashiriki tarehe sawa ya kuzaliwa naye. Alieleza kuwa mpenziwe na mtoto wao wapo salama na buheri wa afya.

"Alikuja siku ya  kuadhimisha kuzaliwa kwangu. Tungependa kuwafahamisha nyie kuwa mtoto na mama yake wanafanya vizuri na wanatunzwa hapa hospitalini. Ni hadithi kubwa ya jinsi mambo yalivyotokea.Hatuwezi kusubiri kuwapeleka katika safari yote. Tunawapenda," Tyler aliandika kwenye Instagram.

Tyler aliambatanisha ujumbe wake na video inayowaonyesha wakiwa wamekaa kwenye kiti kabla ya kufungua mirija iliyofichua  jinsia ya mtoto wao.

Mamia ya wanamitandao wameendelea kuwapongeza wapenzi hao wawili kwa ukurasa mpya wa maisha yao ambao wamefungua.

Wawili hao walitangazia ulimwengu habari za ujauzito wao mwishoni mwa mwezi Machi. Hapo awali walikuwa wamedokeza kuwa mtoto wao atatua duniani mapema mwezi huu  wa Mei.

Georgina Njenga akishirikisha mashabiki wake katika kipindi cha Q&A wiki kadhaa zilizopita alifichua kuwa ujauzito huo sio jambo ambalo walipangia.

Aliweka wazi kwamba yeye na mpenzi wake waliwahi kuzungumzia suala la kupata watoto ila hawakukusudia kutimiza mpango huo hivi karibuni.

"Tumekuwa tukiishi pamoja kwa kipindi cha miaka miwili sasa, kwa hivyo tulikuwa tumezungumzia suala la kupata watoto, lakini haikupaswa kuwa hivi karibuni. Hata hivyo, pia tulikuwa tumekubaliana kuwa ikitokea tutakuwa sawa kupata mmoja," Georgina alimjibu shabiki aliyetaka kujua ikiwa walikuwa wamepanga kupata mtoto.

Malkia huyo mwenye umri wa miaka 21 pia alifichua  hawajakuwa wakitumia mbinu zozote za kupanga uzazi.

Kutoka Radio Jambo, tunawapongeza Tyler na Georgina kwa hatua kubwa ambayo wamepiga ya kuwa wazazi. Tunawatakia kila la kheri katika safari yao mpya.