Rich Mavoko afunguka kuhusu uhusiano wake wa sasa na Diamond, Harmonize

Mavoko aligura Wasafi takriban miaka minne iliyopita

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo alisema imefikia hatua ambapo amechia Diamond mwenyewe kueleza kuhusu uhusiano wao.

•Mavoko aliweka wazi kuwa yeye na Harmonize ni marafiki na hata huwa wanawazungumza mara kwa mara

HARMONIZE, RICH MAVOKO, DIAMOND PLATNUMZ
HARMONIZE, RICH MAVOKO, DIAMOND PLATNUMZ
Image: FACEBOOK

Staa wa Bongo Richard Martin Lusinga almaarufu Rich Mavoko ameweka wazi kuwa hana uhusiano wa karibu na aliyekuwa bosi wake Diamond Platnumz.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, Mavoko alisema kwa sasa hana chochote cha kuzungumza kumhusu bosi huyo wa WCB.

Mwanamuziki huyo alisema imefikia hatua ambapo amechia Diamond mwenyewe kueleza kuhusu uhusiano wao.

"Nadhani imefika muda waandishi wamuulize huyo mtu. Mimi kwa sasa siwezi kuongea kuhusu huyo jamaa. Siwezi kumwongelea chochote. Simkumbuki. Sijui chochote. Imefika muda kwa yeye kuulizwa. Ni muda wake. Wakati wetu umekwisha," Mavoko alisema.

Mavoko aligura Wasafi takriban miaka minne iliyopita baada ya kutamatisha mkataba wake na lebo hiyo ya Diamond.  Tangu kuondoka kwake amekuwa akifanya muziki kivyake.

Katika mahojiano mengine Mavoko alisema hakuna vidhibiti vyovyote ambavyo Wasafi illiweka kwenye muziki wake licha yake kuondoka.

"Kila kitu changu ni cha kwangu. Sijawahi kusimamishwa kutumbuiza. Sijawahi kuambiwa usifanye hiki. Kila kitu ambacho nimeimba nimeandika mwenyewe, sio wasafi ama mtu yeyote, ni mimi na talanta yangu. Hakuna mtu ambaye anaweza kunizuia kuimba wimbo wowote," Mavoko alisema katika mahojiano na SPM Buzz.

Pia aliweka wazi kuwa hakuna hela zozote ambazo aliagizwa kulipa na lebo ili mkataba wake utamatishwe, kinyume na madai ambayo yamekuwepo.

Mwanamuziki huyo pia amezungumzia uhusiano wake na aliyekuwa msanii mwenzake katika Wasafi, Harmonize.

Mavoko aliweka wazi kuwa yeye na Harmonize ni marafiki na hata huwa wanawazungumza mara kwa mara. Aliweka wazi kuwa hana ugomvi na bosi huyo wa Konde Music Worldwide.

"Sisi ni marafiki. Ni mtu ambaye tunaongea naye mara moja moja kwa sababu tupo kwenye tasnia ya muziki. Tunapopata wakati tunaongea. Kila mtu anaendesha shughuli zake hatuwezi kukutana sana. Tunakaa mbali mbali lakini hatuna shida," Alisema.