(Video) Tazama maoni ya Tarrus Riley kuhusu Wajackoyah kuhalalisha bangi Kenya.

Muhtasari

• "Mimi nafikiri wanadamu ni haramu zaidi kuliko bangi ambayo wameiharamisha" - Tarrus Riley alipoulizwa maoni yake kuhusu Wajackoyah kutaka kuhalalisha bangi.

Tarrus Riley, George Wajackoyah
Image: Instagram

Mwanamuziki nguli kutokea Jamaica, Tarrus Riley hatimaye ametoa wazo lake kuhusu moja kati ya vipengele vya manifesto ya wakili msomi profesa George vWajackoyah cha kuhalalisha ukulima na matumizi ya bangi pindi atakapoteuliwa kama rais wa tano wa taifa la Kenya.

Katika video fupi ambapo ilipakiwa kwenye ukurasa wa Instagram wa Mpashogram, mwanamuziki huyo wa miziki aina ya Reggae aliulizwa wazo lake kuhusu kipengee hicho cha Wajackoyah kinachohusu uhaalalishwaji wa bangi naye pindi tu baada ya kusikia swali kama hilo alionekana kushtushwa pakubwa kwani hakuwa anatarajia gumzo kama hilo linaweza likazuka nchini Kenya, haswa kutoka kwa mgombea urais.

“Tuko na mwaniaji wa rais anaitwa Wajackoyah, anatokea chama cha Roots na moja kati ya vipengee vya manifesto yake ni kuhalalisha bangi nchini. Wazo lako ni lipi kuhusu hilo?” anasikika akimuuliza mwanahabari.

“Kuhalalisha bangi? Sikuwa najua, mimi nafikiri wanadamu ni haramu zaidi kuliko bangi ambayo wameiharamisha na pia mimi sihitaji wanasiasa kuniambia hilo,” Tarrus Riley alijibu kwa mshangao mkubwa.

Tarrus Riley alitua nchini mwishoni mwa wiki jana na alikuwa mmojqa kati ya watumbuizaji wakubwa katika hafla ya World Rally Championship Koroga Festival iliyofanyika mjini Naivasha wikendi iliyopita.

Wengi walikisia kwamba mshangao wake ulitokana na kwamba yeye anakotokea bangi imehalalishwa tena muda mrefu tu kwa hiyo alishangaa kusikia kwamba kumbe mataifa duniani ambapo bado mjadala wa iwapo bangi itahalalishwa au la ungalipo, jambo ambalo alichukizwa nalo haswa baada ya kusikia kwamba limezuka kutokana na mawimbi ya kisiasa nchini.

Ikumbukwe taifa la Jamaica anakotokea Tarrus Riley ni moja ya mataifa duniani ambayo yamehalalisha matumizi ya bangi na asilimia kubwa ya wananchi hutumia bangi kawaida tu pasi na shruti kutoka kwa mtu yeyote.

Wakili msomi profesa George Wajackoyah ameapa kuhalalisha ukulima wa bangi nchini kenya pindi ataakaapoteuliwa kama rais wa Kenya ila katika kampeni zake anasisitiza kwamba ukulima wa bangi hautakuwa kwa matumizi ya ndani bali ni kwa ajili ya kuuza nje ya nchi ili kupata mapato ya kulipa mikopo na madeni ya Kenya ambapo mpaka sasa yanakisiwa kuwa zaidi ya shilingi trilioni 9.