"Najua mimi ni mpango wa kando, lakini acha kupost mkeo kila mara!" Dacha amwambia Akuku

Sandra Dacha na Akuku Danger wamekuwa wakitupiana maneno fiche mitandaoni, baadhi wanahisi mambo hayako sawa baina yao

Muhtasari

• “Najua mimi ni mchepuko wko lakini Manason zingatia jinsi unavyompakia mke wako kwenye mitandao yako,” - aliandika Dacha

• “Babu yangu Akuku Danger alikuwa na wake 264 peke yake. Mnafikiria chenye mimi ninafikiria?” - Akuku alionekana kujibu.

Muigizaji Sandra Dacha, Mcheshi Akuku Danger na familia yake
Image: Akuku Danger (Facebook)

Kama kile ambacho kinaendelea kwenye mitandao ya kijamii ni kielelezo kamili, basi hamna budi kusema kwamba huenda mahusiano ya mchekeshaji Akuku Danger na Sandra Dacha yamevurugika pakubwa.

Hili lilidhihirika wazi juzi wakati Akuku Danger aliporuhusiwa kurudi nyumbani baada ya kuugua ghafla wiki iliyopita kutokana na tatizo lake la kukosa damu mwilini, kwa kimombo Sickle Cell Anaemia.

Mchekeshaji huyo alikuwa na furaha ya kurudia nyumbani na kuonana na familia yake ambapo alipakia picha ya pamoja na mwanamke aliyesemekana kuwa mkewe halisi pamoja na mtoto na kufuatisha kwa maneno kwamba ana furaha sana kujumuika na familia tena baada ya kuondoka hospitalini.

Sandra Dacha ni kama hakufurahia kitendo hicho cha Akuku Danger ambaye jina lake halisi ni Mannerson Ochieng kupakia picha za mkewe halisi kila mara na aliamua kujibu mipigo kwa kuandika kwenye instastory yake akimtaka Akuku kukoma kupakia picha za mkewe.

Dacha pia alikiri kwamba anajua yeye ni mchepuko wa Akuku lakini haifai mchekeshaji huyo kupakia picha ya mkewe halisi kila mara kwani ni sawa na kumtupia tope usoni.

“Najua mimi ni mchepuko wko lakini Manason zingatia jinsi unavyompakia mke wako kwenye mitandao yako,” aliandika Dacha kwenye Instagram yake.

Katika kile kiichoonekana kama ni kumjibu Dacha, Akuku Danger naye aliandika kwa njia ya ucheshi na utani huku akidokeza kwamba huenda anafuata nyendo za babu yake ambaye jina lake lilikuwa maarufu ilipofahamika kwamba alikuwa na wanawake wengi na wajukuu zaidi ya elfu moja.

“Babu yangu Akuku Danger alikuwa na wake 264 peke yake. Mnafikiria chenye mimi ninafikiria?” aliandika Akuku Danger huku wengi wakikisia kwamba huenda alidokeza kuwa na wake zaidi ya mmoja kama babu yake na kwa hiyo Dacha asiwe na nongwa.

Uvumi kuhusu Dacha na Akuku kuwa katika mahusiano ulizuka mwishoni mwa mwaka jana pale ambapo Akuku alilazwa na Dacha kukiri wazi kwamba yeye na mcheshi huyo ni wapenzi, kwa kutumia kauli ambayo ilikuwa maarufu ‘dawa ya balloon ni sindano’ akijifananisha na balloon kutokana na unene wake na Akuku kama sindano kutokana na wembamba wake.

Ila wapo wengine ambao bado hawaamini kwamba wawili hao wamekosana na kuanza kurushiana maneno mitandaoni na kusema kwamba huenda wanafanya mitikasi yao mitandaoni tu kama kawaida kwani wote ni wachekeshaji na waigizaji.

Maoni yako ni yepi?