Wanawake? Mbosso afunguka chanzo halisi cha beef yake na Aslay

Muhtasari

•Mbosso alieleza kuwa urafiki wao ulikatika ghafla baada ya Aslay kum-unfollow kwenye mitandao ya kijamii.

•Alisema kuwa tofauti zake na mwenzake huyo wa zamani zilianza muda usio mrefu baada yake kujiunga na WCB.

Mbosso, Aslay
Mbosso, Aslay
Image: INSTAGRAM

Staa wa Bongo Yusuf Kilungi almaarufu Mbosso amepuuzilia mbali madai kuwa alizozana na Aslay kuhusu wanawake wao.

Akiwa kwenye mahojiano na Wasafi Media, Mbosso alisema hakuna sababu za msingi zilizosababisha ugomvi kati yao.

Alieleza kuwa urafiki wao ulikatika ghafla baada ya Aslay kum-unfollow kwenye mitandao ya kijamii.

"Hakuna hata suala la maana. Ni upuuzi tu! Kitu gani cha maana hapo tulichogombania. Ni upuuzi tu kwamba huyu anafanya kazi zake huku na mwingine anafanya kazi zake huko, ghafla huyo wa huku kakunja na huyo wa huko kaona baas ikakuwa hivo," Mbosso alisema.

Msanii huyo wa WCB alifichua kwamba Aslay alitangulia kwa kujitenga na bendi yao ya YAMOTO ili kuangazia kazi zake pekee yake.

Baadaye, wanabendi wengine; Enock Bella, Beka Flavour na yeye,  walitengana na kila mmoja akaanza kufanya kazi kivyao.

"Aliondoka akaamua kufanya maisha yake akatuacha sisi watatu tunaishi pamoja. Yeye alikuwa na mambo yake, alikuwa anatoa mangoma na sisi wengine tulikuwa tunamsapoti, sisi wengine hatukuwa na mangoma tulikuwa tunamsapoti kwa nafasi yake," Alisema.

Mbosso alisema kuwa tofauti zake na mwenzake huyo wa zamani zilianza muda usio mrefu baada yake kujiunga na WCB.

Mwandani huyo wa Diamond Platnumz hata hivyo alikana kuwa Aslay alimuonea kijicho kwa kuwa alianza kufanya vizuri.

Pia alipuuzilia mbali madai kuwa kuna tofauti zilizopo kati yake na Beka Flavour, ambaye pia alikuwa katika Yamoto Band.

Alisema anatamani sana tofauti zilizopo baina yake na wanabendi wenzake wa zamani wa YAMOTO yaishe.

"Natamani tuwe fiti kabisa," Alisema.