Bahati akanusha kufurushwa, "Sifuna aliahirisha mkutano aliponiona naingia na umati wangu"

Bahati alipuzilia mbali video inayosambazwa na kusema katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna alimaliza mkutano alipomuona amefika.

Muhtasari

• Mkewe Bahati, Diana Marua amemtia msukumo na kumtaka asife moyo kwani njia ya kuingia kileleni huwa na changamoto nyingi.

Bahati
Image: Instagram

Msanii wa kizazi kipya Bahati Kioko ambaye alijitosa kwenye ulingo wa siasa kuwania ubunge wa mathare kwa tikiti ya Jubilee amejitokeza na kupuuzilia mbali madai na video ambayo imekuwa ikisambazwa mitandaoni kwamba alifurushwa katika mkutano mmoja wa kisiasa kwenye eneo bunge hilo.

Kupitia Instagram yake, Bahati amepakia video inayodaiwa kuwa na tukio ambalo alifurushwa katika mkutano huo na kuipuzilia mbali huku akimgeuzia kibao katibu mkuu wa chama cha ODM, Edwin Sifuna kuwa yeye ndiye alikatisha mkutano ghafla baada ya kuona Bahati akikuja na kundi lake likimsherehekea kwa kelele na vifijo huku wakiimba jina lake.

“Sifuna na Rafiki yake Aliyepoteza uchaguzi mara mingi Walipomwona MBUNGE WA MATHARE ANAYEINGIA - BAHATI KIOKO amefika na Umati wa watu ulikuwa Ukitaka kunisikia nikizungumza... Waliamua Kumaliza Mkutano ghafla, kinyume na matakwa ya wananchi wa Mathare” aliandika Bahati kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Msanii huyo ambaye alionekana bado kujipa moyo hata baada ya kuambiwa na viongozi wa vuguvugu la Azimio la Umoja kwamba ajitoe na kumuunga mkono mbunge wa sasa Anthony Oluoch ambaye analenga kukitetea kiti hicho kwa tikiti ya chama chas ODM, alisema kwamba yeye anaamini kwa Mungu ambaye halali na majaaliwa watu wa Mathare mnamo Agosti 9 watajitokeza kwa wingi wa siafu kumchagua kama mbunge wao.

Mkewe, Diana Marua ambaye muda wote amekuwa akimpa shavu na msukumo wa kuendelea na azma yake ya kuwaongoza watu wa Mathare pia alitoa maoni yake kwenye video hiyo ambapo alimsifia mumewe na kusema yeye ni kama wimbi kubwa lisilojua kusimamishwa kwa nguvu zozote.

“Wewe ni Nguvu isiyoweza kupuuzwa!!! Njia ya kwenda juu haiwezi kufikiwa bila upinzani. Endelea Kusukuma... Mungu yupo nawe, Watu wa Mathare tayari wanajua ni nani aliye Bora kwao,” alitilia mkazo mkewe.

Hii si mara ya kwanza msanii Bahati anajipata katika wakati mgumu kutoka kwa viongozi wa Azimio la Umoja kwani mapema mwezi Aprili uvumi uliibuka kwamba amenyimwa cheti cha Jubilee kuwania ubunge ambapo alitokwa na machozi hadharani, ila baadae akakubaliwa kuwania baada ya kukabidhiwa cheti, lakini kama wanavyosema wenye midomo, safari yake kuelekea bungeni bado haijapata mwanga kwa sababu ya visingiti na ukungwi mkubwa ulioko mbele yake kutoka kwa baadhi ya viongozi katika muungano wanaohisi msanii huyo anafaa kuachia na kumuunga mpinzani wake mkono.