Olwenya Maina:Mauti yazima aliyekuwa sauti ya 'Radio Jambo'

Marehemu alitambulika kwa jina la utani 'A turkan" wakati akihudumu Radio Jambo.

Muhtasari

•Jamii ya Radio Africa Group inamkumbuka Wilfred Olwenya kwa mchango mkubwa ambao alitoa kwa muda mrefu.

•Wale waliopata nafasi ya kufanya kazi naye wamesema aliungana nao vizuri na alifanya kazi yake ipasavyo.

Marehemu Wilfred Olwenya Maina
Marehemu Wilfred Olwenya Maina
Image: HISANI

Wapenzi wa filamu za Kenya wanaendelea kumuomboleza muigizaji Wilfred Olwenya Maina almaarufu 'Otis'.

Olwenya ambaye anatambulika zaidi kutokana na filamu 'Nairobi Half Life' alizirai na kufariki dunia Jumatatu jioni.

Wakenya wengi wanaofahamu kazi za muigizaji huyo wamemuomboleza hasa kwa kupitia mitandao ya kijamii.

Jamii ya Radio Africa Group pia inamkumbuka marehemu kwa mchango mkubwa ambao alitoa kwa muda mrefu.

Kwa kipindi cha takriban miaka mitano ,Olwenya alifanya kazi katika idara ya utayarishaji akihudumu kama msanii wa sauti wa kituo chetu cha Radio Jambo.

Kwa mujibu wa wafanyikazi wenzake wa zamani, marehemu alitambulika kwa jina la utani 'Aturkan" wakati akihudumu Radio Jambo.

"Kuna wakati alikuja akiwa amechoka sana, alikuwa ametoka kutengeneza filamu. Hakuweza kutamka jina Turkana vizuri. Alishinda akisema Aturkan kumaanisha A Turkana. Hilo likawa jina lake la studio," Aliyekuwa mfanyikazi mwenzake alisema.

Idara ya utayarishaji katika Radio Africa imemtaja marehemu kama "mtu mwenye nafsi nzuri na mwenye furaha."

Wale waliopata nafasi ya kufanya kazi naye wamesema aliungana nao vizuri na alifanya kazi yake ipasavyo.

"Alikuwa na sauti nzuri. Sauti yake ilikuwa kila kitu na alikuwa jamaa mzuri. Kusema kweli alikuwa na nafsi nzuri," Timu ya utayarishaji ilisema.

Marehemu alitengeneza sauti za vipindi na za matangazo ya kibiashara  katika Radio Jambo hadi mwaka jana.

"Alikuwa sauti ya Radio Jambo. Alifanya kila kitu hapa," Mfanyikazi mwenzake wa zamani alisema.

Baadhi ya wafanyikazi wengine wa Radio Africa wakiwemo watangazaji Mbusii na Maina Kageni pia wamemuomboleza marehemu.

"Pumzika kwa amani ndugu yangu, ulicheza nafasi kubwa kwa kazi yetu," Mbusii alimuomboleza marehemu kupitia Instagram.

 Maina Kageni kwa upande wake alimsherehekea kipaji kikubwa cha Olwenya na sauti yake maalum iliyopongezwa na wengi.

"Tutakukumbuka hapa katika Radio Africa... wewe ni miongoni mwa sauti bora sana Afrika Mashariki.... mwigizaji mkubwa, mwenye kipaji cha hali ya juu!!!! Tutakumbuka uhusika wako bora katika filamu ya Nairobi Half-life... jinsi ulivyobadili mchezo, Big Boss!!!!!!" Maina Kageni alimuomboleza marehemu kupitia Facebook.

Sote katika Radio Jambo na Radio Afrika kwa ujumla tunamtakia marehemu mapumziko ya amani. Mola awatie nguvu wanafamilia wake pamoja na mashabiki wake.