Nyerere: Tutaomba mamlaka ifanye likizo siku ya harusi ya Billnas na Nandy

Billnas na Nandy walivishana pete ya uchumba miezi sita iliyopita.

Muhtasari

• Nyerere alisema ndoa ya wawili hao haiwezi kuvunjika hata aje shetani wa chuma.

Mwenyekiti wa ndoa ya Billnas na Nandy, Steve Nyerere
Screenshot Mwenyekiti wa ndoa ya Billnas na Nandy, Steve Nyerere
Image: Clouds FM

Muigizaji Steve Nyerere kwa mara nyingine tena baada la zogo la kuteuliwa kwake kama msemaji wa wasanii, ameibuka na jipya kabisa ambalo ndilo gumzo la vijiweni.

Nyerere safari hii amekuja na habari mpya kuhusu harusi iliyosubiriwa sana kati ya wasanii nandy na mchumba wake wa muda mrefu, Billnass.

Muigizaji huyo mcheshi amefichua kwamba Nandy na Billnass walimfuata na kumbembeleza kwamba pasi na yeye basi ndoa haitafana na hivyo kumtaka kuwa mwenyekiti wa shughuli nzima.

Anasema kwamba chini yake kama mwenyekiti wa harusi ya wasanii hao, hakutafanyika harusi ya kimasihara bali kutafanyika bonge la harusi ambayo kwake alisema itaitwa ‘Wedding’

“Harusi wanafanya watu wa kawaida, lakini hii chini yangu tutafanya kitu inaitwa Wedding, haijawahi fanyika kama hiyo tangu uhuru watu wamekuwa wakifanya harusi, hii itakuwa wedding,” alisisitiza Nyerere.

Katika taswira ambayo msanii huyo alijaribu kuielezea ni kwamab itakuwa bonge la harusi ambapo pia alidokeza kwamba wataiomba mamlaka ruhusa kipindi hicho cha harusi wananchi wote wapewe likizo ya kitaifa ili kuhudhuria na kufuatilia harusi ya wasanii Nandy na Billnass.

“Kama harusi hii ikifanyika Ijumaa, ikianza Ijumaa hadi Alhamisi tuombe mamlaka basi iwe siku kuu ili watu wote waweze kushiriki,” alisema kwa utani Nyerere.

Alisema kwamba kutokana na ukubwa wa atakayeolewa, ambaye ni Nandy, na kwa vile anajiita mwana wa mfalme Afrika basi nchi nyingi zimemtafuta kwa njia ya simu kutaka kupewa kibsli kushiriki katika mahudhurio ya harusi yenyewe.

Akionekana kuligusia suala la watu maarufu kuoana na kisha kuachana muda mchache baadae ambalo limekuwa ni tatizo kubwa katika ndoa za watu mashuhuri, Nyerere alisema kwamab kwa vile yeye ni mwenyekiti, kuachana kwa wawili hao ni mwiko.

“Na mimi nikiwa kama mwenyekiti suala la hawa watu kuachana haliwezekani. Ile ni ndoa ya kikristo, kufa na kuzikana, Hata aje shetani wa chuma, hawa kuachana haiwezekani,” alifoka Nyerere.