Msanii Ringtone ambaye juzi ametoa tangazo kubwa la kuihama injili na kuanza kuimba nyimbo za kidunia, haswa za mapenzi sasa anasema kwamba kibarua chake kikuu ni kumpoteza kabisa msanii nguli wa bongo fleva, Diamond Platnumz kutoka kusikika humu nchini.
Ringtone alisema kwamba wasanii walioko kwenye sekta hiyo ya tungo za kidunia kwa muda mrefu sana wameshindwa kuhimili na kumiliki Sanaa ya muziki wa Kenya mpaka kuwaachia nafasi kubwa wasanii kutoka nje kusikika humu nchini utadhani kwao.
Amesema yeye pindi tu atakapoingia kwenye studio kutema madini yake kwenye kipasa sauti basi huo ndio utauwa mwisho wa msanii Diamond na wenzake kusikika nchini Kenya, kwani nyimbo zake za kimapenzi zitateka anga na kuhanikiza katika janibu zote kila kona nchini Kenya.
“Sijasema nimeenda nyimbo za kidunia. Nilisema nitaanza kuimba nyimbo za mapenzi ambazo wasanii kama kina Otile Brown wameshindwa hata kumtoa Diamond Kenya, kwa hiyo mimi nataka kumuangamiza na kumtoa. Si kumuangamiza kimwili bali kimuziki,” Ringtone aliapa.
Msanii huyo kwa muda mrefu amekuwa akisema kwamba yeye ana utajiri mkubwa sana kumliko Diamond Platnumz ambapo amekuwa akisema yeye hana mali mingi yakiwemo magari ya kifahari na majumba ya kumezewa mate katika mitaa yenye utulivu wa kutukuka jijini Nairobi.
Ringtone pia alieleza wazi kwamba hakusema ameasi injili basi tu kuimba ndicho kitu ameacha na kusema kwamba mambo mengine atakuwa akiyafanya kama kawaida tu ikiwemo kuwasapoti wale ambao wamebaki kwenye injili.
“Mimi sijawacha wokovu, nimeacha tu kuimba. Lakini mambo mengine nitaendelea kufanya kama sadaka, fungu la kumi, nasapoti wale wanafanya huduma, wale wahubiri lakini mambo ya Injili nimeacha kwa sababu wanadada wananisumbua sana. Nimeacha ili wamrudie Mungu,” alisema Ringtone.